01 August 2012
Michuano ya Super 8 yaingia doa *Simba kuingiza timu ya vijana
Na Zahoro Mlanzi
WAKATI Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), likiikunia kichwa michuano mipya ya Super 8 Cup, Klabu ya Simba, imesema kutokana na kubanwa na programu zao, itapeleka timu ya vijana (U-20) katika michuano hiyo.
Pia klabu hiyo, imesema TFF imepokea ombi lao la kutaka timu zitakazoshiriki michuano hiyo zikutane kujadili namna zitakavyoshiriki ambapo sasa wanapanga tarehe ya kukutana.
Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Geofrey Nyange 'Kaburu' alisema hawatapeleka kikosi chao kitakachoriki Ligi Kuu Bara kutokana na kubanwa na progamu za 'Pre season'.
"Kiukweli hatupo tayari kupeleka timu ya wakubwa kwani kwa hivi sasa tupo katika maandalizi ya msimu mpya na pia kiufundi itakuwa ngumu, tumeshiriki michuano miwili tofauti hivi karibuni, tunahitaji timu ijipange na pia wachezaji wapumzike," alisema Kaburu.
Alisema michuano hiyo haipo katika kalenda na imekuja katika mazingira yasiyotarajiwa huku wakishindwa kushirikishwa, zaidi wanasikia kupitia vyombo vya habari.
Kaburu alisema kutokana na hilo, ndiyo maana wakaiandikia barua TFF kuhusu michuano hiyo kutaka ufafanuzi zaidi kwa kushirikisha klabu zote zitakazoshiriki, jambo ambalo alidai TFF inapanga ni lini itakutana na timu hizo.
Alisema michuano hiyo inaonekana ina lengo la kuinufaisha TFF, kwani hata mapato inaonekana timu shiriki inachukua asilimia chache huku shirikisho hilo likipata asilimia kubwa, kitu ambacho si sahihi.
"Hata kama tukifikia muafaka katika hilo la mapato, lakini sisi (Simba) tumekubaliana ni bora tupeleke kikosi chetu cha pili katika michuano hiyo kuliko kikosi cha kwanza, kwani tutakosa muda wa kujiandaa na Ligi Kuu," alisema Kaburu.
Mbali na hilo, pia alizungumzia maandalizi ya Simba Day ambayo hufanyika kila mwaka Agosti 8, ambapo alisema yanaendelea vizuri na kwamba bado wanahangaika kutafuta timu kutoka nje watakayocheza nayo siku hiyo.
Alisema timu nyingi hivi sasa bado zinaendelea na ligi za nyumbani kwao, lakini watajitahidi kuleta timu iyakayokuwa na ushindani na bora katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment