26 July 2012

Maliasili: Hatujakalia ripoti yoyote


Na Stella Aron

WIZARA ya Maliasili na Utalii, imesema hakuna ripoti ya wanyama ambayo imekaliwa na Wizara hiyo kuhusu suala la uchunguzi wa tuhuma za watumishi wanaodaiwa kuhusika na utoroshaji wanyama kama inavyodaiwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini.


Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Msemaji wa Wizara hiyo, Bw. George Matiko, ilisema si kweli kwamba Wizara imekalia ripoti inayohusu suala hilo.

Alisema taarifa iliyotoka kwenye vyombo vya habari, ilisema Wizara hiyo ilikabidhiwa ripoti ya utoroshwaji wanyama jambo ambalo halina ukweli wowote.

Alisema kamati iliyoundwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuchunguza tuhumu za watumishi waliohusika na utoroshaji huo katika Uwanja wa Ndege mkoani Kilimanjaro (KIA), haikukabidhiwa kwa Wizara hiyo.

“Habari hii haina ukweli wowote, Waziri wa Maliasili na Utalii alishapewa ripoti hii na anaifanyia kazi,” alisema Bw. Matiko na kuongeza kuwa, suala la kutoroshwa wanyama hao linashughulikiwa na mamlaka nyingine za Serikali na liko mahakamani kwa sasa.

Alisema si wajibu wa Wizara hiyo kulitolea taarifa suala hilo ambapo kamati iliyoundwa na Katibu Mkuu ni kwa matumizi ya ndani ya Wizara sio ya kusambazwa.

No comments:

Post a Comment