26 July 2012

Makalla: Wizara kukamilisha sera maendeleo ya michezo



SERIKALI katika mwaka wa fedha 2012/13, inatarajia kukamilisha Marekebisho yanayohusu Sera ya Maendeleo ya Michezo toleo la mwaka 1995.

Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Bw. Amos Makalla, aliyasema hayo bungeni mjini Dodoma jana, wakati akijibu swali la Mbunge wa  Kinondoni, Bw. Idd Azzan (CCM).


Katika swali lake, Bw. Azzan alitaka kujua ni lini Serikali itaweka sawa sera ya michezo na mkakati walionao kuhuwisha Sheria ya Baraza la Michezo nchini.

Akijibu swali hilo, Bw. Makalla alisema Wizara ilipoanza kufanya mchakato huo, waligundua kuna wadau wengi waliokuwa mikoani na wilayani ambao walikuwa hawafahamu vyema Sera inayohusu  Maendeleo ya Michezo na Sheria ya Baraza la Michezo Taifa.

“Baada ya kugundua kasoro hii, Wizara yangu ilichukua hatua za makusudi kushirikisha wadau wa michezo katika mikoa na Wilaya ili kuwaelimisha, kupata maoni na mapendekezo yao kuhusu maendeleo ya michezo,” alisema.

Akizungumzia suala la Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT), ya mwaka 1967 na marekebisho ya sheria namba 6 ya mwaka 1971, alisema mchakato wake umeanza kwa kuainisha maeneo yenye kasoro na kupokea maoni kutoka kwa wadau.

Bw. Makalla alisema rasimu ya mchakato huo itakamilika baada ya kufanyika marekebisho yanayohusu sera ya maendeleo ya michezo ili kuepuka mkinzano wa sera na sheria.

No comments:

Post a Comment