26 July 2012

Mbunge ataka ufafanuzi madini yanayochimba, kufanyiwa tafiti



MBUNGE wa Muhambwe, Bw. Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi), ameitaka Serikali kueleza kiasi cha madini yaliyochimbwa katika tafiti mbalimbali, baada ya kuchimbwa yamepelekwa wapi na Serikali imechukua hatua gani kuhakikisha hayaibiwi.

Akijibu swali hiyo bungeni mjini Dodoma jana, Naibu Waziri Wizara ya Nishati na Madini Bw. George Simbachawene, alisema Wizara hiyo inatoa leseni za utafutaji mkubwa wa madini katika maeneo mbalimbali nchini.

Alisema kuwa utafutaji huo unalenga kujua kiasi cha mashapo ya madini ambayo yanaweza kuchimbwa kibiashara.

Aliongeza kuwa, kiasi cha madini yanayochimbwa na kuchukua sampuri za udongo, mchanga au mawe, hupelekwa katika maabara za ndani na nje ya nchi ili kujua kiwango cha madini kwenye eneo husika ambapo nchini Tanzania shughuli hizo hufanywa na GST, SEAMIC na SGS.

Alisema sampuri zinazochukuliwa katika maeneo ya utafutaji madini husafirishwa kwa utaratibu wa vibari  ambavyo hutolewa kwenye ofisi za madini zilizoko karibu na eneo la utafiti.

“Hakuna kampuni au mtu yeyote anayeruhusiwa kusafirisha sampuri za madini au madini yoyote bila kupata kibali kutoka mamlaka husika kama Ofisi ya Madini na TRA.

“Kampuni au mtu yoyote ambaye itabainika kufanya hivyo, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao, Maofisa madini hufanya ukaguzi wa maeneo ya utafiti na uzalishaji madini wakishirikiana na Wakala wa Mkaguzi wa Madini kuhakiki maendeleo ya shughuli ili kudhibiti vitendo vinavyokiuka sheria,” alisema.

Aliongeza kuwa, kutokana na sheria ya madini mwaka 2010,  kampuni zinazofanya utafiti wa madini hutakiwa kuwasilisha taarifa  za utendaji kazi kila robo mwaka ambazo huakikiwa na Wizara kwa ushirikiano wa Wakala wa Jiolojia nchini (GST), ili kujua kazi zinazofanywa na kampuni hizo,” alisema.


No comments:

Post a Comment