06 March 2012

Wanne familia moja wafa kwa moto

*Ni mama na watoto watatu, baba na mtoto walazwa
Na  Patrick Mabula, Bukombe

WATU wanne wa familia moja wakazi wa Ushirombo, Wilaya ya Bukombe, mkoani Shinyanga, wamefariki dunia baada ya kuteketea kwa moto na wengine wawili kunusurika.

Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki saa saba usiku wakiwa wamelala nyumbani kwao. Waliokufa ni Bi. Yunisi Burushi (31), na watoto wake watatu Katukura Mwenyeji (7) Gress Mwenyeji (4) pamoja na Roda Mwenyeji ambaye ana mwaka mmoja na nusu.

Wakizungumza na Majira, mashuhuda wa tukio hilo walisema mtoto mmoja wa familia hiyo Mzuri Mwenyeji (12) na baba yao Bw. Mwenyeji Katukura, waliungua sehemu mbalimbali za miili yao na wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya Ushirombo.

Akisimulia tukio hilo, mtoto Mzuri alisema siku hiyo baba yake alikuwa amewasha jenereta na kuangalia televisheni hasi saa sita usiku alipoamua kulizima na kuliingiza ndani sebureni.

“Baada ya baba kuingiza jenereta, tulikwenda kulala lakini sebuleni tuliwasha mshumaa ambao tuliacha ukiwaka hivyo usiku saa saba tulishangaa kuona nyumba ikiwaka moto,” alisema.

Mtoto huyo ambaye anasoma darasa la tano katika Shule ya Msingi Bomani, alisema walichukua hatua za kujiokoa wakisaidiwa na majirani waliovunja mlango ili kuwatoa lakini ilishindikana hivyo walilazimika kuvunja dirisha la chumbani kwa wazazi wao na kumuokoa yeye na Bw. Katukura lakini wengine waliteketea.

Mchungaji wa Kanisa la AICT, Zacharia Kilezu aliwataka waumini kuwaombea kwa Mungu kwani kifo chao kimetokana na mateso.

Kwa Upande wake, Askofu wa kanisa hilo Dayosisi ya Shinyanga, John Nkora alituma salamu za rambirambi kwa ndugu na jamaa wa familia hiyo kwa niaba ya kanisa.






No comments:

Post a Comment