JITIHADA mbalimbali zimekuwa zikifanywa na wanaharakati wa masuala ya jinsia nchini kuhakikisha vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto vinakoma lakini juhudi hizo hazijafanikiwa.
Baadhi ya taarifa zinaeleza kuwa, katika baadhi ya maeneo wanawake wameendelea kufanyiwa ukatili wa kupigwa, kubakwa, kuumizwa, kufukuzwa katika familia na kunyimwa fursa ya kutoa mawazo yao katika jamii.
Tatizo la mfumo dume nalo linachangia ukatili wa kijinsia kwa wanawake ambapo wanaume wengi ndio waamuzi wa kila kitu katika familia na kupanga matumizi.
Hali hiyo imewafanya wanawake wengi kujiona dhaifu mbele ya wanaume hivyo kujikuta wakibaki nyuma na kukosa uamuzi juu ya miili yao na kusababisha wasichana wadogo kuozwa katika umri mdogo.
Baadhi ya mila zimekuwa zikiwafanyia wanawake ukeketaji kwa madai kuwa, utamwezesha kupiga hatua moja ya kuondoka katika utoto. Kimsingi mila hizo, zimewaathiri wanawake wengi hata kusababisha vifo na kuathirika kisaikolojia.
Wanawake wananyimwa fursa ya kumiliki ardhi au nyumba pindi baba katika familia anapofariki na kusababisha mjane kufukuzwa hata kupigwa na kunyang’anywa mali.
Sisi tunasema kuwa, mfumo wa kiutawala nchini hauna uwiano mzuri wa kijinsia ndio maana baadhi ya wananchi na wanasiasa hawakusita kuweka wazi kuwa, katiba ya nchi ina upungufu mkubwa na haikidhi matakwa, maslahi ya wananchi.
Upungufu huo ni pamoja na katiba husika kutoa mamlaka makubwa kwa mhimili wa utawala kuliko mihimili mingine ya mahakama na bunge. Hali hiyo inatoa mianya ya ukiukwaji wa haki za binadamu hasa kwa upande wa wanawake na watoto.
Tatizo la ajira nalo limesababisha ongezeko la umaskini hivyo ukatili wa kijinsia kuendelea kushika kasi. Tumeshuhudia na kuona tatizo la kuyumba kwa uchumi ambalo limesababisha maelfu ya Watanzania kupunguzwa kazi katika ajira rasmi.
Imani yetu ni kwamba, hali hiyo imesababisha kundi kubwa la wanaume kukosa uwezo wa kuhudumia familia zao. Hali hiyo inachangia ukatili wa kijinsia.
Tatizo la watoto waishio katika mazingira hatarishi ni kubwa hivyo kila mwananchi awajibike kuhakikisha uhai, ulinzi, matunzo, makuzi na maendeleo ya watoto yanazingatiwa.
No comments:
Post a Comment