01 March 2012

Wanafunzi 8 wafa maji, abiria 5 ajarini

Na Pamela Mollel, Arusha
WANAFUNZI  nane wa Shule ya Msingi Pipaya, iliyopo Wilaya ya Ngorongoro, mkoani Arusha, wamefariki dunia baada ya kusombwa na maji wakati wakijaribu kuvuka mto wakitokea shuleni kwenda nyumbani.

Akizungumza na Majira jana, Kamanda wa Polisi Mkoa hapa Thobias Andengenye, alisema tukio hilo lilitokea Februari 27 mwaka huu, saa 11:30 jioni katika Kijiji cha Kiyaya.

Aliwataja waliokufa kuwa ni mwanafunzi wa darasa la saba Olonana Mosirori (13), Nemao Faraji (14) na Lapaine Lengukuwi (14) wote wa darasa la tano, Lekinyani Eliakimu (11) darasa la pili na Kisiyaya Mbalinoto(13), darasa la sita ambao ndio miili yao ilipatikana.

Wengine ambao miili yao bado haijapatikana ni Ponyangusi Mbalau (12) mwanafunzi wa darasa la tano na Logoi Oleiki(11) darasa la pili.

“Tukio hili limechangiwa na mvua kubwa iliyonyesha jana (juzi), saa tisa alasiri katika Wilaya hii na kusababisha maji kujaa kwenye mito mbalimbali hali iliyochangia wanafunzi kushindwa kuvuka.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi wilayani hapa kwa kushirikiana na wananchi wanaendelea kutafuta miili mingine mitatu ambayo bado
haijapatikana ambapo ile iliyoopolewa, imekabidhiwa kwa ndugu zao kwa ajili ya mazishi.

Wakati huo huo, askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Kikosi cha  977 Tanganyika Packers, Bw. Joseph Simsokwe (37), amekutwa amekufa pembezoni mwa korongo baada ya kusombwa na maji ya mvua katika eneo la Njiro kwa Msola, nje kidogo ya Jiji la Arusha.

Tukio hilo limetokea juzi saa tatu asubuhi ambapo polisi waliokuwa doria, waliukuta mwili huo ukiwa umekwama kwenye korongo.

Kamanda Andengenye alisema polisi walifika eneo hilo baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia na baada ya kuuchunguza walibaini ulikuwa wa askari wa JWTZ  ambaye alikutwa na jeraha kubwa la mshono katika mguu wa kulia linalodaiwa kutokana na ajali ya pikipiki.

Kwa mujibu wa majirani na marehemu, walisema askari huyo alikuwa mtumiaji wa pombe kupita kiasi ambapo siku ya tukio anadaiwa alikuwa amekunywa pombe ambayo ilisababisha ashindwe kuvuka mto na kusombwa na maji.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospital ya Mkoa Mount Meru, kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Mwandishi wetu Daud Magesa, kutoka Mwanza anaripoti kuwa, 
watu watano wamekufa na wengine 11 kujeruhiwa katika ajali
iliyohusisha magari mawili kwenye Kijiji cha Bulula, Kata ya Nyangune, Tarafa ya Kahangara, Barabara ya Mwanza-Musoma Wilaya ya Magu, mkoani Mwanza.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Liberatus Barlow, alisema ajali hiyo ilihusisha basi dogo la abiria ambapo chanzo ni dereva wa gari aina ya Noah yenye namba za usajili T 716 BMV kugeuka ghafla barabarani akiwa katika mwendo kasi na kugongana na basi hilo.

Alisema basi hilo lenye namba za usajili T 655 BDP mali ya Kampuni ya Zakaria Wambura, lilikuwa likiendeshwa na Bw. Aziz Hassan ambapo gari aina ya Noah lilikuwa ikitokea Magu mjini kwenda jijini Mwanza.

“Katika ajali hii watu watano wamekufa papo hapo ambao walikuwa katika gari ya Noah akiwemo dereva, abiria 11 waliokuwa katika basi la Zakaria, walijeruhiwa 10 kati yao, walikimbizwa Hospitali ya Wilaya ya Magu kwa matibabu.

“Majeruhi mmoja kati ya hao 11, Bw. Mbarouk Taka (52), mkazi wa Vingunguti Dar es Salaam, amevunjika mkono wa kuliana amekimbizwa Hospitali ya Rufaa Bugando,” alisema.

Aliwataja marehemu waliotambuliwa majina yao kuwa ni dereva wa Noah Bw. Deus Kengele (42), mkazi wa Kiloleli, Wilaya ya Ilelema mfanyabiashara Bw. Peter Lubisha (45), fundi umeme Bw. Emmanule Kapesa (30) na mwingine aliyetambuliwa kwa jina moja la Bw. Mwinyi mkazi wa Igoma Wilaya ya Nyamagana ambapo marehemu mmoja hajatambuliwa.







No comments:

Post a Comment