Salim Nyomolelo na Grace Ndossa
WAKATI wabunge wengi wakishinikiza kuongezewa posho kutoka sh. 70,000 hadi 200,000, imebainika kuwa baadhi yao hawaelewi kutafsiri lugha ya bajeti ya Serikali, kwa kuandikwa kwa kiswahili cha kitaalam.
Akizungumza katika kipindi cha mahojiano cha dakika 45 kilichotangazwa na Televisheni ya ITV juzi, Waziri wa Ofisi ya Rais na Utawala Bora, Bw. Mathias Chikawe, alisema kutokana na wabunge wengi kutoelewa lugha hiyo, itabidi iwekwe kwenye kiswahili Rais.
"Baadhi ya wabunge hawaielewi bajeti, hivyo itakuwa vigumu kwa mwananchi wa kawaida kuielewa," alisema Bw.Chikawe na kuongeza kuwa kutokana na hali hiyo wabunge wanashindwa kusaidia wananchi kuielewa.
Alisisitiza kuwa wananchi wanatakiwa kujua bajeti ya nchi yao, lakini kutokana na lugha ambayo inatumika kuiandika ni vigumu wao kuielewa kwa sababu baadhi ya wabunge hawaielewi lugha inayotumika kuiandaa.
Katika hatua nyingine Bw. Chikawe alikiri kuwa fedha nyingi zinazotengwa kwa ajili ya miradi mbalimbali ya halmashauri nchini, zinapotea bila ya kuwafikia walengwa, hali inayochangiwa na mchakato mrefu wa kuzifikisha kwa walengwa.
Kutokana na hali hiyo alisema Serikali imekuwa ikipoteza fedha nyingi kwenye halmashauri nchini hivyo kusababisha miradi iliyopangiwa kukwama.
Alisema asilimia 75 ya bajeti hupolekwa katika halmashauri nchini, hasa katika sekta ya elimu ambapo mafanikio ya utekelezaji wa miradi hayaonekani badala yake fedha hizo zinaliwa na wajanja wachache.
"Kuna mianya mingi ya upotevu wa fedha hapa katikati bila ya kuwafikia walengwa na hatujui zinafanya kazi gani,"alisema Bw.Chikawe
Alisema wanashangazwa na matokeo ya kidato cha nne kuendelea kuwa mabaya zaidi, wakati halmashauri zinatengewa fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu msingi na sekondari.
Akizungumzia kuhusu mikakati ya iliyowekwa ili kudhibiti hali hiyo, Bw.Chikawe alisema wameanzisha mfumo mpya wa utawala bora, ambapo utawashirikisha wananchi kupata taarifa za miradi mbalimbali pamoja na bajeti itakayotengwa ili waweze kufuatilia na kutoa taarifa pale, ambapo utekelezaji hautofanyika.
Alisema mifumo ya uwazi itasaidia zaidi kuwapa wananchi taarifa, ambapo wanatakiwa kujua na kushirikishwa katika kila mchakato wa maendeleo ili waweze kutoa taarifa pale ambapo mambo hayatakwenda sawa.
Akizungumzia suala la uwajibikaji alisema kuna mchakato wa kupewa ahadi hewa ambapo unapewa muda wa kujibiwa bila ya utekelezaji wowote kufanyika.
"Unaomba fedha hazina unaambiwa usubiri baada ya siku saba utapewa lakini siku hizo zinapita hakuna utekelezaji wowote,"alisema
No comments:
Post a Comment