*Akiri sakata la muswada wa katiba kumtikisa
*Aeleza kilichomfanya asaini haraka haraka
Peter Mwenda na Willbroad Mathias
RAIS Jakaya Kikwete amekiri kuwa mgomo wa madaktari ulitikisa taifa na makovu yake yatabaki katika kumbukumbu za historia ya taaluma ya tiba hapa nchini.
Rais Kikwete aliyasema hayo jana katika hotuba yake kwa taifa na kukiri kuwa tayari amekabidhiwa na Waziri Mkuu, Bw.Mizengo Pinda, taarifa ya Kamati aliyounda kushughulikia madai ya madaktari.
"Kuanzia kesho Serikali itaifanyia kazi taarifa hiyo na kuamua ipasavyo kulingana na uwezo uliopo," alisema Rais Kikwete na kuongeza;
"Nawaomba madaktari kuwa na moyo wa subira. Napenda kutumia fursa hii kuwahakikishia ndugu zetu madaktari na watumishi wengine wote wa sekta ya afya kwamba Serikali inatambua, inajali na kuthamini kazi wazifanyazo na mchango wao katika kulinda na kudumisha afya za wananchi wa Tanzania."
Katika hotuba hiyo Rais Kikwete alitoa pole kwa wananchi na hasa wagonjwa nchini kwa mateso waliyoyapata katika kipindi cha mgomo.
"Ni matumaini yangu kuwa hali kama ile haitajirudia tena katika nchi yetu," alisema Rais Kikwete.
. Mauaji ya Songea
Mbali na mgomo wa madaktari alielezea kusikitishwa na mauaji ya Songea yale yanayohusishwa na imani za ushirikina na yale ambayo yalitokea kwenye maandamano.
"Napenda kutumia nafasi hii kuelezea masikitiko yangu kwa vifo hivyo na kutoa pole na rambirambi zangu na za wananchi wa Tanzania kwa ndugu wa marehemu wetu hao.
Tupo pamoja nanyi katika misiba hii mikubwa na majonzi. Napenda kuwahakikishia wananchi wa Songea kwamba Serikali kupitia vyombo vyake vya usalama imekuwa inafanya na itaendelea kufanya uchunguzi wa kina wa mauaji haya mpaka wahusika wote wapatikane na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria," alisema Rais Kikwete.
Mabadiliko ya Katiba
Akizungumzia hatua yake ya kusaini muswada wa mabadiliko ya katina, Rais Kikwete alisema katika mazungumzo yake na viongozi wa vyama vya siasa waliokwenda kumuona Ikulu, aliwaeleza ugumu aliouona kuhusu kuacha kutia sahihi muswada huo na kuurudisha tena Bungeni kujadiliwa upya.
"Nilichelea kuliingiza taifa letu katika mgogoro mkubwa wa kisiasa na kikatiba usiokuwa wa lazima. Mgogoro ambao tunaweza kuuepuka kwa kutumia njia nyingine za kikatiba na kisheria kufikia malengo yale yale," alisema Rais Kikwete na kuongeza;
"Kitendo cha mimi kukataa kutia sahihi kingejenga chuki kwa upande wa wabunge walio wengi ambao waliujadili muswada na kuupitisha.... wengeweza kuhisi wamedharauliwa na kuonekana hawana thamani."
Alipongeza vyama vya siasa vya CHADEMA, CUF, NCCR-Mageuzi na CCM na Baraza la Taifa la Asasi Zisizokuwa za Kiserikali kwa uelewa wao na ushirikiano.
"Kwa kweli, jinsi hali ilivyokuwa huko nyuma, hatuna budi kushukuru na kujipongeza. Ni matumaini yangu na rai yangu kuwa tutaendeleza ushirikiano na utamaduni huu wa mazungumzo tuliouanzisha na kuutumia katika hatua zingine zinazofuata," alisema na kuongeza;
Kikwete, usidanganye watu kuhusu kusaini ule mswada. Rejea hotuba yako uliyoitoa mbele za wazee wa Dar es Salaam, ambayo ilikuwa ni maelekezo tosha kwa wabunge wa chama chako. Posho walizoanza kujichotea akina Makinda zilikuwa ni ahadi kwao kabla hujawakana kwa kauli zako za utatanishi baada ya kuona kwamba wananchi hawakubaliani na mambo yote mawili - mchakato wa katiba na posho za wabunge. Kiongozi gani wewe unayefanya maamuzi kwa kuangalia upepo unapoelekea kwanza? Huna 'conviction' na jambo lolote la maslahi ya nchi yako. Umeonyesha udhaifu mkubwa sana. Mungu atujalie tu, umalize salama ngwe yako hii bila ya misukosuko mikubwa katika huu muda wako uliosalia.
ReplyDelete