Na Florah Temba, Kilimanjaro
SERIKALI mkoani Kilimanjaro imezinyooshea kidole halmashauri za wilaya mkoani humo kwa kuwa chanzo kikubwa cha uharibifu wa mazingira katika maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye misitu ya asili.
Hali ambayo ilidaiwa imesababisha mabadiliko makubwa ya tabia nchi na kuyeyuka kwa barafu ya Mlima Kilimanjaro.
Akizungumza kwenye kikao cha dharura cha Kamati ya Ushauri mkoani humo (RCC), Mkuu wa mkoa, Bw. Leonidas Gama jana alisema, halmashauri za wilaya ni wahusika wakubwa katika uharibifu wa mazingira na zinapaswa kuwajibika katika hilo.
Bw.Gama alisema, katika halmashauri za wilaya sheria za mazingira zipo lakini kumekuwepo hakuna usimamizi wa sheria hizo na hiyo ni kutokana na watendaji wake kuwa sehemu ya tatizo hilo la uharibifu na hivyo kushindwa kudhibiti uharibifu huo.
“Katika suala hili la uharibifu wa mazingira naomba niseme mchawi wetu ni halmashauri, kwani uharibifu unafanyika, lakini hakuna mwenye habari na hili ni kutokana na watendaji wetu kuanzia wakurugenzi, madiwani, viongozi wa kata kuwa sehemu ya tatizo hili," Bw.Gama.
Alisema, jitihada za kudhibiti uharibifu wa mazingira kwa sasa si nguvu ya soda na kwamba mtendaji ambaye anaona hawezi kwenda sambamba na yeye ni bora akatafuta sehemu ya kwenda kwani asipoondoka mwenyewe atamfukuza.
“Sheria za mazingira zipo na kila mmoja anazifahamu sasa naomba kila mmoja atekeleze wajibu wake na kama hawezi aondoke, kama alikuwa amejisahau sasa arudi relini na vivyo hivyo kama hawezi kurudi relini atafute pa...kwenda kwani mimi nitamfukuza aende akanishtaki kwa waziri," alisisitiza Bw.Gama.
Hata hivyo wadau mbalimbali wa mazingira katika kikao hicho walisema, suala la uharibifu wa mazingira katika Mkoa wa Kilimanjaro kwa sasa ni janga hivyo kunahitajika nguvu za ziada na za makusudi ili kurudisha uoto wa rasilimali za mazingira katika Mkoa wa Kilimanjaro kama ilivyokuwa hapo awali.
Bw.Jackob Mushi ambaye ni miongoni mwa wadau hao alisema kila halmashauri ya wilaya ina sheria za mazingira, lakini cha kushangaza zimekuwa hazitekelezwi na badala yake zimekuwa zikiliwa na 'mende' hivyo ni wakati wa kila mmoja kuanzia na watendaji kubadilika na kuondokana na utendaji kazi wa kimazoea.
“Lazima tujiulize kwa nini uharibifu unafanyika? Wakati sheria zipo, hapa ni lazima kuna mkono wa watumishi sasa tuondokane na siasa katika kutekeleza hili na tufanye kwa vitendo kwani hata maneno ya Mungu yamesema imani pasipo matendo imekufa,”alisema Bw. Mushi.
Kwa upande wake Katibu wa CCM mkoani Kilimanjaro, Bw. Steven Kazidi alisema, suala la utunzaji wa mazingira halina itikadi za kisiasa hivyo ni wajibu wa kila mmoja bila kujali itikadi zake kuhakikisha anasimama kukemea uharibifu wa mazingira na kuyahifadhi.
Bw.Kazidi alisema, sheria za mazingira zipo wazi hivyo ni wakati wa kuhakikisha zinafuatwa na kuondokana na hali ya kuoneana aibu kwani kikubwa ambacho kimekuwa kikichangia tatizo la uharibifu kuzidi kuwa kubwa ni kuzidi kuoneana haya.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambnaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Hai, Bw.Freeman Mbowe alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro kwa jitihada za makusudi za kulinda na kuhifadhi mazingira ikiwa ni pamoja na kutangaza kuwachukulia hatua wale watakaoharibu mazingira.
Pamoja na pongezi hizo, Bw. Mbowe alishauri kuanzishwa kwa kodi maalumu kwa watalii wanaopanda Mlima Kilimanjaro ambayo itakusanywa na halmashauri kupitia Hifadhi ya Kilimanjaro KINAPA.
Alisema, fedha hizo zitasaidia kulinda na kuhifadhi mazingira ya Mlima Kilimanjaro ambapo nusu ya mapato hayo yataelekezwa moja kwa moja kwenye mfuko wa kulinda mlima huo na nusu zitaelekezwa kwenye shughuli za maendeleo ya jamii.
Hata hivyo kikao hicho cha dharura ambacho kiliitishwa na Mkuu wa mkoa kikiwa na agenda moja ya kujadili vyanzo vya uharibifu wa mazingira na kuweka mikakati ya kudhibiti tatizo hilo kiliazimia mambo mbalimbali ikiwemo kufungia vibali vya ukataji miti ya asili kwa ajili ya mbao pamoja na sheria za hifadhi mazingira na misitu zisimamiwe kikamilifu kuanzia ngazi ya kijiji, wilaya hadi mkoa.
Maazimio mengine ni viongozi na watendaji wa serikali wa ngazi zote wanaopatikana na uharibifu au ujangili wa biashara za mazao ya misitu wachukuliwe hatua stahiki bila kuonewa aibu pamoja na viwanda vyote vinavyotumia kuni kama nishati na vinavyopasua mbao vichunguzwe ili kuona malighafi hiyo inatoka wapi
No comments:
Post a Comment