01 March 2012

Benki ya Africa Tanzania yatoa zawadi

Na Peter Mwenda

BENKI ya Africa Tanzania imetoa zawadi mbalimbali kwa mwanariadha, Sarah Kavina aliyepeperusha vyema bendera ya Tanzania katika mbio za kimataifa zilizofanyika hivi karibuni Bamako nchini Mali.

Akizungumza kabla ya kukabidhi zawadi ya fedha taslimu, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Africa Tanzania Ammish Owusu-Amoah, alisema benki yake iliwapeleka wanariadha wawili wa Tanzania, Sarah Kavina na Andrea Mathiya ambao wamefanya vizuri.

“Tunayofuraha kuwajulisha kuwa, Sarah Kavina aliibuka kwa kupeperusha bendera ya Tanzania vyema katika mashindano ya kimataifa ya benki Afrika "Bank of Africa International Marathon’ ya kilomita kumi kwa upande wa wanawake ambapo nchi 14 zilishiriki ikiwemo Ufaransa,” alisema Owusu-Amoah.

Alisema mashindano hayo hushirikisha nchi ambazo benki hiyo inafanya kazi, ambapo Tanzania ilishiriki kwa awamu ya pili na imeweza kupata ushindi kwa upande wa mbio za wanawake kwa awamu zote kupitia mwanariadha Sarah.

Mkurugenzi huyo alisema benki yake pia imempatia zawadi Andrea Mathiya kwa kushiriki kwake vizuri katika mashindano hayo, lakini hakurudi na ushindi na kumtaka kuzidi kufanya vyema katika mchezo huo ili mwaka ujao aweze kushiriki tena na kupata ushindi.

Alisema Benki yake itazidi kuwaandaa Watanzania kama njia ya kusaidia kuibua na kukuza vipaji katika mchezo huo, ili waweze kushiriki hata katika mbio za kimataifa zikiwemo za Olimpiki.


No comments:

Post a Comment