07 March 2012

Tuzo ya Rais kwa wawekezaji kuchochea maendeleo nchini


Na Reuben Kagaruki
KWA takribani kipindi cha miaka 14 iliyopita, Tanzania imekuwa na ongezeko kubwa la  miradi ya madini na viwanda katika utafutaji na uchimbaji wa madini ya madini na utafutaji wa gesi na mafuta ya petroli. Miradi hiyo imekuwa chini ya kampuni binafsi.

Pamoja na ongezeko hilo kubwa la uwekezaji, bado kumekuwepo na kilio kikubwa kutoka kwa wananchi hasa wanaoishi maeneo jirani na kampuni za uwekezaji.

Kilio hicho kinatokana na jamii  inayozunguka maeneo hayo kutonufaika na uwekezaji huo. Sekta hizo  zimekuwa zikitajwa kuchangia kiasi kidogo katika pato la Serikali ikilinganishwa na sekta nyingine.

Kwa mujibu wa sera ya madini ya mwaka  2009, sekta ya madini inakua  kwa asilimia  15.7 kila mwaka na kuchangia Pato ya Taifa (GDP) kwa kiasi cha asilimia 2.7 kwa mwaka.

Kwa upande wa ukuaji wa sekta ya nishati ya gesi na umeme ukuaji wake ni kwa asilimia asilimia 8.4  kwa mwaka na kuchangia  pato la Taifa kwa kiasi cha asilimia  2.1. kipindi hicho hicho.

Hali hiyo inadaiwa kusababishwa utegemezi wa uagizaji wa vifaa vya kuchimba madini kutoka nje ya nchi  ambayo vinagharimu kampuni husika fedha nyingi za kigeni.

Kutokana na hali hiyo Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na jukwaa la wadau katika sekta ya madini (MISF),kwa kupitia mpango wa Uwajibikaji katika Mahusiano ya Kijamii na Usawa (CSRE), wameamua kuandaa tuzo ya Rais,ili kuhakikisha sekta hiyo inawanufaisha Watanzania wanaozunguka maeneo zinapozalishwa nishati hizo.

Waandaaji hao wanasema kuwa tuzo  hiyo ya rais itakuwa kichocheo  na  itaongeza kasi katika sekta ya madini sekta ya kampuni kufanya biashara zao kwa faida lakini pia kuborsha hali ya endelevu ya kiuchumi katika jamii.

Tuzo hiyo ilizinduliwa na Rais Jakata Kikwete wiki iliyopita. Wakati wa uzinduzi wa tuzo hiyo Rais Jakaya Kikwete aliziagiza kampuni za ndani na nje ambazo zinajihusisha na sekta ya madini, gesi na mafuta kununua bidhaa zinazozalishwa nchini pamoja na kuziwezesha jamii zinazozunguka maeneo ya uwekezaji ili zifaidike na raslimali za nchi yao.

Katika hotuba yake Rais Kikwete anasema wawekezaji hao pamoja na misaada watakayotoa kwa wananchi wahakikishe wanalipa kodi ya Serikali kwa wakati ili nchi ifaidike na raslimali zake.

“Hii italeta mahusiano mazuri kati ya wawekezaji na wananchi wanaozunguka miradi ya uwekezaji...bila kufanya hivyo mahusiano baina ya pande mbili hizo yanaweza kuwa mabaya na kusababisha kuwepo kwa misuguano ya mara kwa mara,” anasema Rais Kikwete.

Rais anashutumu baadhi ya wawekezaji kununua baadhi ya bidhaa nje ya nchi, wakati bidhaa hizo zinapatikana nchini tena kwa wingi.

Anatoa mfano namna alivyoenda katika hoteli moja ya kitalii hapa nchini na kukuta maji ya kunywa yanaagizwa nje ya nchi, jambo ambalo hakufurahishwa nalo na kugoma kuyanywa.

“Kwa nini muagize maji nje ya nchi wakati tuna uhai, Ndanda, Kilimanjaro na Masafi? Haya mambo hayawafurahishi wananchi,” anasema Rais Kikwete na kuongeza; “kuna bidhaa na huduma nyingi mnaweza kununua hapa nchini na hii ni moja ya kukuza uchumi wa wananchi wetu.”

Rais anasisitiza kuwa wananchi wanahitaji kuona faida zinazoonekana kwa macho zinazotokana na kuwepo kwa sekta hiyo ya uziduaji.

“Watu watajiuliza wanapata nini, dhahabu yetu inachukuliwa, kampuni hizi zina misamaha ya kodi, lakini hata hawatuungi mkono kiuchumi kwa kununua bidhaa zetu. Hawatakuwa na chochote katika biashara hii,” anasema Rais Kikwete.

Rais Kikwete anatoa mfano kwa makampuni yanayozalisha sukari kama mfano wa wawekezaji wazuri ambao wanawezesha wananchi wanaowazunguka kupitia kilimo cha miwa ambao baadaye wanawauzia tena.

“Uzalishaji wa kampuni za sukari haufanani na ule wa kampuni za uziduaji, lakini suala la uwekezaji kiuchumi ndilo la muhimu,” anasema Rais Kikwete.

Anasisitiza kuwa wakati umefika wakati wananchi wanahitaji kuona kwa macho faida zinazotokana na kuwepo kwa uwekezaji katika sekta ya uziduaji bila kufanya hivyo kunaweza kuleta misuguano kwenye maeneo ya uwekezaji.

“Katika maeneo ya uwekezaji ni lazima tuwe na mpango wa wewe faidika na mimi nifaidike kati ya wawekezaji na jamii zinazowazunguka,” anasema Rais Kikwete.

Rais Kikwete anasema kuwa ili kuhakikisha kwamba,sera ya madini na nishati ya mwaka  2009 na 2003  inatekelezwa vyema na Serikali  Wawekezaji, na Jumuiya ya  kutoa ushirikiano na sekta nyingine katika kuleta maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.

Kwa upande wake Waziri wa Nishati na Madini, Bw. William Ngeleja anasema sekta ya ugagaduzi wa madini imekuwa na mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Anasema pamoja na mafanikio hayo, bado kuna changamoto ya namna wananchi wanaozunguka katika maeneo ya uwekezaji wanaweza kufaidika na kuwepo kwa miradi ya uwekezaji katika sekta hiyo.

“Tuzo ya Rais ambayo lengo lake ni kuhamasisha wawekezaji wawe karibu na wananchi wanazowazunguka itakuwa inatolewa kila mwaka kwa wawekezaji wakubwa, wa kati na wadogo katika sekta hii ya uziduaji,” anasema, Bw.Ngeleja.

Anasema tuzo hiyo imeandaliwa kwa pamoja kati ya Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na Jukwaa la Wadau wa Sekta ya Madini, Mafuta na Gesi (MISF).

Bw. Ngeleja anaeleza kwamba MISF inahusisha kampuni ambazo zimesaini hati ya makubaliano (MoU) na wizara kuanzisha jukwaa ambalo litakuwa na jukumu la utetezi wa sera, utafiti, elimu pamoja na namna ya kutatua migogoro kati ya wawekezaji na wanajamii.

Anasema tuzo hiyo ya Rais inatarajiwa kuhamasisha sekta za madini, gesi na mafuta kushirikiana na jamii katika kuboresha uchumi wa maeneo ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wanajamii wa maeneo husika.

Bw.Ngeleja anasema ili kuhakikisha sera ya madini ya mwaka 2009 na 2003  inatekelezwa na Serikali, wawekezaji na jumuiya lakini kuwepo na ushirikiano na sekta nyingine ili kuleta maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.

Akizungumzia mpango huo wa CSRE, unaoratibiwa na kampuni ya Excutive Solution kupitia kitengo cha matukio na mahusiano kwa mwaka mzima mpaka tuzo hizo zitakapotolewa Novemba mwaka huu, Rais Kikwete, Bw. Ngeleja anasema utasaidia kuhamasisha mahusiano kati ya  wachimbaji madini, mafuta na gesi na makampuni ya utafutaji miradi katika maeneo mbalimbali ya nchi na jamii jirani.

Anasema pia mpango huo utasaidia kuongeza ufahamu kwa umma juu ya shughuli za madini na nishati, ushirikiano wa madini na sekta za nishati na nyingine za kiuchumi, kujenga uwazi zaidi katika majukumu pamoja na kujenga imani na umiliki kwa jamii, ubora kwa uelewa na kujenga mtazamo chanya juu ya sekta za ndani ya nchi.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Jukwa la Wadau wa Sekta ya Madini,Mafuta na Gesi, Catherine Lyombe, anasema tuzo hiyo itachangia kuboresha uendeshaji wa biashara kwa njia ambayo itachangia maendeleo ya kijamii na mazingira ya kuanzishia biashara.

Wanasema CSRE ina dhamira ya kuendeleza sera ambazo zitaunganisha mazoea ya kuwajibika katika shughuli za kila siku za biashara, na kuripoti juu ya mafanikio yaliyopatikana kwa kutekeleza vitendo hivi.


No comments:

Post a Comment