JANA Waziri Mkuu Bw. Mizengo Pinda, alikutana na waandishi wa habari kuzungumzia hatua mbalimbali zilizofanywa na Serikali ili kufikia muafaka wa madai ya madaktari ambao.
Bw. Pinda alilazimika kuzungumzia sakata hilo baada ya Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), kutoa saa 72 kwa Serikali iwe imewafukuza kazi Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hadji Mponda na Naibu wake Dkt. Lucy Nkya.
Katika maelezo yake, Bw. Pinda alisema madai ya madaktari ambayo yapo katika ripoti iliyowasilishwa kwake na tume aliyounda yanazungumzika ila sharti la kuwaondoa watendaji wakuu wa Wizara hiyo kwa lazima , limevuka mipaka.
Alisema suala la Rais Jakaya Kikwete kupewa saa 72 zinazoisha kesho (leo), awe amewafukuza watendaji hao wakuu wa Wizara, ili meza ya mazungumzo iweze kuendelea yeye haliafiki.
Aliongeza kuwa, hata Rais Kikwete hawezi kuafiki sharti hilo kwani viongozi hao wana kofia ya kisiasa hivyo taratibu za kuwaondoa zinapaswa kufuatwa. Wakati Bw. Pinda akisisitiza hilo, MAT inasema sharti hilo ni muhimu kutekelezwa na Serikali.
Sisi tunatoa wito kwa madaktari kusitisha mgomo uliopangwa kuanza leo badala yake wakae meza moja na Serikali ambayo imeonesha dhamira ya kutatua madai yao.
Migomo inachangia kutoweka kwa utulivu, maelewano, amani, kupoteza maisha ya wananchi wasio na hatia, kupunguza tija, uzalishaji, kuzorotesha ustawi na ukuaji wa uchumi Kitaifa.
Vita ya maneno kati ya madaktari na Serikali, imechangia kutikisa Taifa na kuathiri huduma za matibabu katika baadhi ya hospitali nchini hivyo jambo muhimu ni pande husika kukaa mezani, kuangalia mambo yanayokubaliana na kufikia muafaka.
Lengo la mazungumzo ni kuokoa maisha ya wagonjwa ambao wanakabiliwa na hatari kubwa kukosa tiba. Tunaomba busara itumike ili nchi yetu isiingie katika historia mbaya.
Tunatambua umuhimu wa taaluma ya udaktari kwa umma na ufinyu wa rasilimali za nchi ambazo pengine ndio kikwazo cha Serikali kushindwa kuwalipa watumishi wake vizuri.
Tofauti zozote kiutendaji au kiutawala, haziwezi kuondolewa bila pande husika kukaa mezani kuzijadili ili kupata mwafaka kwa faida ya Watanzani wote.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment