Na Zahoro Mlanzi
KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imesema chombo pekee kitakachoweza kumrudisha aliyekuwa Katibu Mkuu wa FAT sasa TFF, Michael Wambura katika masuala ya michezo nchini ni Mahakama ya Usuluhishi wa Masuala ya Michezo (CAS) pekee.
Mbali na hilo, kamati hiyo pia imekana taarifa zinazotolewa katika baadhi ya vyombo vya habari kwamba wanamuonea mdau huyo wa soka nchini huku vingine vikidai wanamuogopa kwa kusema wanavyafanya kazi kwa mujibu wa katiba na kanuni zilizopo na si vinginevyo.
Akiyatolea ufafanuzi masuala mbalimbali yaliyomuhusu Wambura katika chaguzi alizoomba kuwania uongozi zikiwemo Uchaguzi Mkuu wa TFF 2008, Uchaguzi wa Klabu ya Simba 2010 na wa Chama cha Soka Mara (FAM) mwaka jana Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Deogratius Lyatto alisema mambo mengi yamezungumzwa kuhusu Wambura lakini ukweli utabaki kama ulivyo.
Alisema hakuna kamati itakayoweza kufanya kazi kwa matakwa ya mtu fulani ili kumuonea mtu fulani au kumnyima haki mtu fulani ila kamati inafanya kazi kwa mujibu wa kanuni zilizotungwa na Kamati ya Utendaji ya TFF.
"Kamati ya Uchaguzi TFF ilimuengua Wambura katika Uchaguzi Mkuu wa TFF 2008 akiwa anawania Umakamu wa Kwanza wa Rais kutokana na kutokidhi matakwa ya uadilifu, lakini hakuishia hapo alikata rufaa kwa Kamati ya Rufaa ya TFF, hata hivyo kamati hiyo ilipitia nyaraka mbalimbali zilizowasilishwa na kujiridhisha kwamba Wambura kweli hakuwa muadilifu," alisema Lyatto.
Alisema baada ya uamuzi huo, chombo pekee kitakachoweza kubadilisha uamuzi huo ni CAS endapo Wambura atakata rufaa huko kwani katika kanuni zao zinaeleza wazi wanapaswa kutekeleza yatakayoagizwa na chombo hicho.
Alisema pia suala hilo liliibuka pia katika Mkutano Mkuu wa TFF 2007 ambapo mkutano huo uliamua kutokana na nyaraka zilizowasilishwa za ripoti ya ukaguzi wa mahesabu ya FAT/TFF kwa 2002 mpaka 2004, ilijiridhisha kwamba ni kweli Wambura alifanya ubadhirifu, hivyo afikishwe mbele ya vyombo vya dola.
Alisema sekretarieti ilifanya kazi yake kama ilivyoagizwa na mkutano mkuu na kulipeleka suala hilo kwa Jeshi la Polisi na baadaye jeshi hilo lilithibitisha kupokea barua hiyo na kumfungulia mashitaka kwa kosa la wizi akiwa mtumishi.
"Kamati yetu inaheshimu maamuzi ya mkutano mkuu wa TFF na hadi sasa haijaarifiwa kimaandishi na chombo chochote kama suala hilo limefikia ukomo wa aina yoyote, hivyo anashangaa kwanini Wambura anaendelea kujihuisha na masuala ya michezo," alisema Lyatto.
Pia alisema aliondolewa katika uchaguzi wa Simba kutokana na kutokuwa na sifa ya kuwa mgombea kwakuwa si mwadilifu lakini kutokana na hilo aliamua kufungua kezi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kusimamisha uchaguzi kitendo ambacho ni kinyume na katiba ya Simba, TFF ibara ya 12(2)(e) na katiba ya FIFA ibara ya 64(2).
Alisema kutokana na kitendo hicho, pia klabu ya Simba ilimsimamisha uanachama Wambura na mpaka sasa TFF haijapokea taarifa yoyote kutoka kwa klabu hiyo kama imemrudisha kwani uamuzi wa kumrudisha unafanywa na Mkutano Mkuu wa klabu hiyo.
Mbali na hilo, Wambura aliwania tena uongozi katika Uchaguzi Mkuu wa FAM nafasi ya uenyekiti lakini pia Kamati ya Uchaguzi ya FAM ilimuondoa kutokana na sababu zile zile za uadilifu na kupeleka masuala ya michezo mahakamani.
Alisema kutokana na hali halisi ilivyo na katiba za vyama vyote kufanana, hata akiendelea kugombea kazi ni hiyo hiyo ila anaweza kusafishwa na CAS pekee kwani ndicho chombo kitakachoweza kutengua maamuzi hayo.
Aliongeza anajua kuna baadhi ya vyombo vya TFF vilishughulikia masuala ya uchaguzi kinyume na matakwa ya katiba ya TFF na kanuni za uchaguzi, hawatakubali hali hiyo itokee tena na watahakikisha wanakuma makini zaidi.
No comments:
Post a Comment