01 March 2012

Taifa Stars kama kawa

Wabaniwa na 'mamba' wa Msumbiji

 Na Elizabeth Mayemba

TIMU ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars), jana ilibanwa mbavu Msumbiji 'Mambas' katika mechi ya awali ya kuwania kucheza fainali za Mataifa ya Afrika, zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.

Msumbiji ndiyo ilikuwa kupata bao dakika ya 22 kupitia kwa Clesio Bauque, ambaye alimnyang'anya mpira Abdi Kassim 'Babi' na kumchambua kipa Juma Kaseja.

Stars baada ya kufungwa bao ilicharuka na kuliandama lango Msumbiji, ambapo juhudi zao zilizaa matunda dakika ya 42 baada ya kusawazisha bao hilo kupitia kwa Mwinyi Kazimoto kwa shuti kali akiwa nje ya 18.

Awali Stars ilifanya mashambulizi mfululizo ambapo dakika ya 15, John Bocco alishindwa kufunga bao baada ya kupata pasi safi kutoka kwa Nizar Khalfan, lakini shuti lake likapanguliwa na kipa wa Msumbiji.

Taifa Stars pia ilishindwa kutumia nafasi ilizozipta dakika za 16, 28 na 37 kupitia kwa Babi na Vicent Barnabas ambao mashuti yao yalipanguliwa na kipa wa Msumbiji.

Msumbiji ilizinduka dakika ya 37 na kufanya shambulizi kali kupitia kwa Bauque ambaye alipiga shuti kali lililopanguliwa na Kaseja.

Kipindi cha pili Stars iliwatoa Nizar Khalfan, Babi na Barnabas na nafasi zao kuchukuliwa na Mrisho Ngassa, Salum Abubakari 'Sire Boy' na Hussein Javu

kuingiza kwa wachezaji hao kuliiongezea uhai timu hiyo, ambayo ilifanya mashambulizi mfululizo langoni mwa Msumbuji kila mara lakini washambuliaji wake walishindwa kutumia nafasi walizopata.

Msumbiji nayo iliwatoa Jeremias Stoe, Joao Mzive na Eduado Jumise na kuwaingiza Carlos Chimomole, Zainadine Jonior na Luis Vaz.

Dakika ya 75 Ngassa alikosa bao ambapo shuti lake liligonga mwamba baada ya kupokea pasi ya Sure Boy, Stars ilikosa bao lingine dakika 78 kupitia kwa Bocco ambaye alipiga shuti hafifu lililodakwa na kipa.

Wachezaji wa Stars itabidi wajilaumu katika mechi hiyo, baada ya kupata nafasi nyingi ambazo walishindwa kuzitumia.

Dakika za lala salama kama si ustadi wa Kaseja, Stars ingejikuta inafungwa bao la pili baada aya beki Agrey Moris, kupiga pasi fyongo iliyomkuta mshambuliaji wa Msumbiji ambaye alitaka kufunga, lakini Kaseja akamnyang'anya mpira miguuni.

ends....


No comments:

Post a Comment