01 March 2012

Bonanza la waandishi kutumia mil. 60/-

Na Zahoro Mlanzi
KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL), imetoa sh. milioni 60 kwa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) ajili ya kudhamini bonanza la waandishi wa habari hizo, linalotarajiwa kufanyika Machi 24, mwaka huu Msasani Club, Dar es Salaam.

Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa kutangaza udhamini huo, Mkurugenzi wa Uhusiano wa Jamii na Sheria wa kampuni hiyo, Stephen Kilindo alisema wameamua kudhamini kutokana na kuheshimu mchango mkubwa unaotolewa na wanahabari.

''Tumeamua kutoa kiasi hicho cha fedha kutokana na uhusiano mzuri tuliokuwa nao kati yetu na wanahabari, hivyo tunawaomba wanahabari wajitokeze kwa wingi siku hiyo ili kulifanya bonanza lifane,'' alisema Kilindo.

Naye Mwenyekiti wa TASWA, Juma pinto aliishukuru kampuni hiyo kwa udhamini wao na kuiomba wawe pia wanasaidia katika semina mbalimbali zinazoendeshwa na chama katika kutoa mafunzo mbalimbali kwa wanahabari.

Alisema udhamini unaotakiwa katika semina ni mdogo, ikilinganishwa na wa bonanza, hivyo aliwaomba wawe pia wanatenga bajeti kwa ajili ya suala hilo.

"Tunaomba TBL itufikirie katika hili la semina, kwani huwa tunapata shida sana kupata udhamini ukifikia wakati wake kwani bajeti yake huwa haizidi sh. milioni 15," alisema Pinto.

Pia Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya bonanza hilo, George John alisema maandalizi yanakwenda vizuri na kwamba tamasha la mwaka huu litakuwa na michezo mbalimbali na pia masumbwi yatakuwepo baada ya kupata maombi kutoka kwa watu mbalimbali.

No comments:

Post a Comment