28 February 2012

Zaki hatihati kuivaa Yanga *Aumia goti, madaktari wahaha kumtibu

Na Charles Mateso
WAKATI Yanga ikitarajiwa kuondoka nchini keshokutwa kwenda Cairo, Misri kwa ajili ya mechi yake ya marudiano dhidi ya Zamalek, timu hiyo imeingia katika mshituko baada ya mshambuliaji wake mahiri, Amr Zaki kuumia goti.

Timu hizo zinatarajiwa kukutana Jumamosi katika mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, ambao unatarajiwa kuchezwa katika Uwanja wa Chuo cha Kijeshi huku mashabiki wakiwa hawaruhusiwi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mtandao wa ahram jana, Zaki alianza pia kusumbuliwa na misuli na hivyo kuamua kuondoka katika mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika juzi, lakini baadaye ikabainika ameumia pia goti, hivyo anatarajiwa kupimwa rasmi ili kujiridhisha kama atacheza katika mchezo huo wa Jumamosi au la.

Daktari wa Zamalek, Ayman Farid alithibitisha hilo na kusema ndani ya saa 48 watahakikisha wanampima Zaki, ili kuona kama ataweza kucheza katika mchezo huo muhimu kwao.

“Zaki atalazimika kufanyiwa vipimo vya afya yake ndani ya saa 48 ili kuona kama ameumia mno au ni maumivu ya kawaida tu.

“Kipimo cha kwanza kimeonesha jeraha alilonalo si kubwa, lakini mchezaji huyu anatakiwa afanyiwe vipimo vingine ili kuona kama atakuwa na uwezo wa kucheza dhidi ya Yanga,” aliuambia mtandao huo.

Zaki alirejea ndani ya kikosi hicho baada ya kuwa nje kwa miezi kadhaa kutokana na mgogoro wa mshahara, ambapo aliisaidia Zamalek kutoka sare ya bao 1-1 na Yanga katika mchezo wa awali.

Hii si mara ya kwanza kwa Zaki kujikuta akisumbuliwa na maumivu, kwani hivi karibuni aliwahi kukosa mechi kadhaa za Ligi Kuu kabla haijasimamishwa.

Maumivu ya goti yanayoonekana kumsumbua Zaki kwa muda mrefu zaidi sasa.

Kuumia kwa Zaki kunaweza kupunguza furaha ya kocha Hassan Shehata, ambaye alijitapa kurejea uwanjani kwa Ahmed Hossam ‘Mido’ aliyetakiwa apunguze uzito.

Mido alitakiwa apunguze uzito wake kwa kilo nane, ambapo aliamua kufanya kweli zaidi baada ya kupunguza kilo 11, hivyo kumfurahisha mno Shehata.

Zamalek iliyotwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika mara tano, kwa sasa ndio imerejea rasmi katika michuano ya kimataifa huku ikitaka taji hilo kwa mara nyingine toka ifanye hivyo mara ya mwisho mwaka 2002.

Katika hatua nyingine, mechi hiyo itakayochezwa Uwanja wa Jeshi jijini Cairo, itaanza saa 12 jioni kwa saa za Misri.


No comments:

Post a Comment