08 March 2012
Siku ya Wanawake na Umuhimu wao katika Jamii
Na Mwandishi wetu
TUANZE Makala haya kwa tafakuli, wangapi miongoni mwetu tumewahi kufikili na kuelewa ni jinsi gani mama zetu walipata taabu wakati kipindi chote cha miezi tisa ya ujauzito?
Ni mateso kiasi gani iliwapasa kuvumilia ili hatimaye kutuleta duniani, kutulea tangu tukiwa watoto mpaka kipindi ambacho tumeweza kujitambua na kusikiliza maagizo na maelekezo ya watu wengine zaidi yao?
Je tumewahi kujiuliza iwapo ni jambo gabi anastahili kufanyiwa mama kwa sababu ya yote waliyotufanyia, au tumewahi kufikili na kuelewa umuhimu wa mama zetu katika maisha yetu?
Majibu ya maswali haya na mengine yanayohusiana yanaifanya Dunia kutambua mchango wao kwa kuadhimisha siku ya Kimataiafa ya wanawake Machi 8 kila Mwaka.
Kupitia matukio na ishara mbalimbali nchi nyingi zimekuwa na maadhimisho maalumu kwa ajili ya kumkumbuka kila mwanamke duniani na kutafakari kwa kina mchango na umuhimu wake katika uwepo wa dunia na mwendelezo wa maisha.
Tanzania ni miongoni mwa Mataifa ambayo yamekuwa mstari wa mbele kutambua mchango wa mwanamke na kuthamini jitihada zake katika kuleta mafanikio na kuhamasisha mabadiliko ya jamii nzima na kwake pia.
Inatambua pia, umuhimu wa mchango wa mwanamke katika shughuli za kisiasa, kijamii na kiuchumi. Kwa sababu hiyo mwaka huu inaungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha siku ya wanawake duniani, kwa pamoja zikibeba ujumbe mkuu “Shirikisha Mtoto wa kike, chochea Maendeleo”
Ni kwa sababu ya kutambua umuhimu wa siku hii, Muungano wa Asasi za Kimataifa na za Kitaifa(CSO) ulioundwa mwaka jana, 2011, baada ya kushiriki kwa pamoja maadhimisho ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Siku ya Wanawake Duniani.
CSO umejitoa kuwa kinara wa harakati za kuimarisha, kutetea na kupigania maslahi ya wanawake kwa kuunganisha nguvu na sera kama familia moja.
Muungano huo, umekuwa unajikita zaidi katika kuhamasisha uwezeshaji wa mwanamke, kupunguza unyanyasaji wa kijinsia, uboreshaji wa huduma kwa wajawazito na afya ya uzazi, ushiriki wa mwanaume katika kumkinga mwanamke na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi na UKIMWI, pamoja na kumwongezea nafasi ya ushiriki na kufanya maamuzi katika jamii.
Kupitia Shirika mwenyeji, Concern Worldwide Tanzania, muungano huu umeandaa maadhimisho ya mwaka huu kwa kuwakumbuka wanawake waishio vijijini ambako upatikanaji wa huduma za kawida bado umeendelea kuwa changamoto iliyokosa ufumbuzi.
Maadhimishao hayo yanayofanyika Wilayani Ngara Mkoani Kagera ni kuamsha ari ya mtoto wa kike na kumjengea hali ya kujiamini, kuongeza juhudi za mwanamke katika kupigania haki za umiliki wa ardhi, kuthamini utu, na kutambua mchango wake katika maendeleo ya jamii.
Muungano huo pia, umejaribu kuchambua kwa undani na kuonesha athari za unyanyasaji wa kijinsia na kuhamasisha mapambano dhidi yake, kuonesha umuhimu wa kuwekeza katika elimu ya mtoto wa kike na kutiliwa mkazo kwa usawa katika jamii.
Juhudi hizi zinalenga kuongeza hamasa kwa wanajamii kufuatia kuwepo kwa mwitikio mdogo uliopo kwa wanajamii katika kukubali mabadiliko na mwendelezo wa mfumo dume.
Mwanamke wa tanzania bila kujali anaishi mjini au kijijini bado anakabiliwa na changamoto za mfumo, amekuwa akitazamwa kama alama ya udhaifu na mtu wa kusikiliza na kutekeleza maagizo kutoka kwa wanamume, hii imesababisha kutokuwepo kwa uwiano mzuri katika nyanja za elimu, ajira na hata katika shughuli za biashara.
Mwanamke ameendelea kutazamwa kama chombo cha mwanamume na nafasi yake ni nyumbani akiwa jikoni na kulea watoto.
CSO inatambua jitihada za Serikali katika miaka ya karibuni, hasa katika awamu ya nne ambapo, wanawake wengi wamepewa nafasi katika nyadhifa za juu za uongozi wa vyama na serikali na utendaji kazi wao umewashangaza wengi.
Kwa sababu hiyo CSO inapenda kuwasilisha kwa jamii kuchukua mifano ya wanawake hao kama kielelezo cha uwezo wa mwanamke na mchango wake katika jamii.
Katika maadhimisho ya mwaka huu, mwitikio wa jamii umeonekana kuongezeka na uelewa wa umuhimu wa siku hii kwa wanajamii, taasisi na mashirika umeongezeka, ndio maana kumekuwa na ushiriki wa wadau mbalimbali kama idara za serikali, Asasi Zisizo za Serikali (AZISE) za kitaifa na za kimataifa.
Asasi hizo ni pamoja na Care International, Oxfam , Action Aid, UDSM Gender Center, CVM Bagamoyo na VSO.
Kupitia maadhimisho hayo, CSO inatoa mwito kwa jamii nzima kutambua kuwa ujenzi wa Taifa lolote Duniani hauwezekani isipikuwa, kwa ushirikiano kati ya mwanamke na mwanamume.
Ili kuamua ni aina gani ya jamii ambayo taifa fulani limekusudia kuwa nayo, ama kiwango cha maendeleo lilichokusudia ni lazima kuwe na ushirikishwaji wa mtoto wa kike kwa kiwango sawa au hata zaidi ya kile cha ushirikishwaji wa mtoto wa kiume.
Hii ni kumaanisha “Ushirikishwaji wa Mtoto wa kike, ni chachu ya Maendeleo katika Jamii” Tunawatakia maadhimisho mema ya siku hii muhimu sana duniani.
Mwisho.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Jamani kwa mara nyingine tunaomba namba ya mtengenezaji wa makala, tuna mambo mengi ambayo tunahitaji muhusika mwenyewe.
ReplyDelete