07 March 2012

Mbatia aibomoa CUF, azoa wanachama wake

Na Mwandishi Wetu, Mtwara
CHAMA cha Wananchi (CUF), kimezidi kuandamwa na jinamizi la kusambaratika baada ya Mwenyeketi wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Bw. James Mbatia, kutikisa ngome ya chama hicho Mjini Mtwara na kuzoa wafuasi zaidi ya 463.

Kati ya waliokimbia chama hicho ni pamoja na aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, Bw. Abdallah Uledi na Kiongozi wa Ulinzi na Usalama Wilaya ya Mtwara, Bw. Mussa Abdallah.

Viongozi hao walitangaza kukihama chama hicho katika mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Bw. Mbatia kwenye Viwanja vya Vigaeni.

Katika mkutano huo, Bw. Mbatia alijikuta akikabiliwa na jukumu kubwa la kugawa kadi za chama hicho na kupokea kadi za wanachama waliohama kutoka CUF.

Baada ya kugawa kadi, Bw. Mbatia alikwenda kufungua tawi jipya eneo la Majengo, Ilala na Mjini Mtwara.

Bw. Mbatia alisema, wakazi wa Mtwara wanaishi maisha magumu kutokana na tabia yao ya kutotaka mageuzi ya kisiasa hivyo aliwataka kubadilika kama ilivyo kwa wakazi wa Mkoa Kigoma, kama wanahitaji maendeleo.

“Wakazi wa Kigoma walikuwa nyuma kimaendeleo, hakukuwa na barabara wala umeme lakini leo hii wanafurahia matunda ya wabunge kutoka upinzani.

“Mkoa wenu kuna utajiri wa kutosha, nyie mna gesi, lakini  haiwanufaishi badala yake inapelekwa Dar es Salaam, mnalima korosho lakini mmebaki maskini kwa sababu hamtaki mageuzi ya kisiasa, mnaichagua CCM kila uchaguzi unapofika,” alisema.

Aliwataka wakazi wa Mkoa huo kuachana na CCM badala yake wajiunge na NCCR-Mageuzi ambacho kinaendesha siasa safi zenye sera nzuri kinyume na vyama vingine.

Alionekana kushangazwa na bei ya zao la korosho ambayo ni kubwa lakini wakulima wanalipwa fedha kidogo.

Akizungumza sababu za kuhama CUF, Bw. Uledi alisema kwa sasa chama hicho kimepoteza mwelekeo.

No comments:

Post a Comment