Waziri wa Ujenzi, Dkt. John Magufuli, akizindua Kituo kipya cha Mabasi madogo ya abiria, eneo la Mbezi Mwisho, Barabara ya Morogoro, Dar es Salaam jana. Wanaoshuhudia tukio hilo kutoka (kulia) ni Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Bw. Harbert Murango, Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mstahiki. Yusuph Mwenda na Mbunge wa Ubungo, Bw. John Mnyika. (Picha na Prona Mumwi)
*Aagiza bomoabomoa ndani ya siku tano
*Ashangiliwa, aambiwa anafaa kuwa rais
Na Goodluck Hongo
WAZIRI wa Ujenzi Dkt. John Magufuli, amempa muda wa siku tano Mkurugenzi wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) awe amebomoa nyumba zote zilizojengwa maeneo ya Hifadhi za Barabara hata kama yana bendera za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwa utekelezaji wa sheria haujali chama.
Dkt. Magufuli alitoa agizo hilo Dar es Salaam jana waakati akifungua kituo kipya cha mabasi kilichopo Mbezi Mwisho.
“Kutokujua sheria si utetezi, kama mnataka upana wa barabara uwe rula, basi twendeni bungeni tukapitishe sheria hiyo na kila moja wetu aizingatie,” alisema Dkt. Magufuli akishangiliwa na wananchi waliokuwa katika uzinduzi huo na kusema “Uwe rais...uwe rais...uwe rais.”
Kauli ya Dkt. Magufuli inaonekana kupingana vikali na ile ya Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, aliyoitoa Machi 6,2011 alipomtaka Waziri huyo kusimamisha bomoabomoa katika Hifadhi za Barabara nchi nzima hadi itakapoamuliwa na Baraza la Mawaziri.
“Rais aliona kwenye sekta ya barabara pana legalega na kumrudisha Dkt. Magufuli kwenye Wizara hii, lakini ameanza kwa spidi kubwa hivyo tumeemwagiza asimamishe oparesheni hii hadi suala hili litakapojadiliwa na Baraza la Mawaziri,” alisema Pinda na kuongeza kuwa, kasi hiyo imeitisha Serikali.
Jana Dkt. Magufuli alisisitiza kuwa, lengo la hatua hiyo ni kuondoa msongamano wa magari unasababishwa na watu kutofuata sheria na kujenga majengo katika maeneo ya Hifadhi za Barabara na kufanya biashara viongozi wakiangalia.
Aliongeza kuwa, hali hiyo inasababisha Serikali kulipa fidia wakati watu wanaovunja sheria husika wakiachwa.
“Nakuagiza Mkurugenzi wa TANROADS, nakupa siku tano kuanzia leo kuvunja vitu vyote hata ikiwa bendera za CCM kwani sheria haina chama, viongozi acheni siasa bali simamieni sheria na bila kufanya hivi, hata wakiletwa malaika nao watakwama kwenye foleni,” alisema Dkt. Magufuli
Alisema Serikali ipo pamoja na wananchi wake kuhakikisha miundombinu inategenezwa ambapo katika mikoa mbalimbali nchini kuna miradi ya barabara ambapo zaidi ya sh. bilioni 240.6 zitatumika kujenga barabara kuanzia Kimara hadi Posta.
Aliongeza kuwa, barabara hiyo itakuwa na vituo vya mabasi 29 kati ya hivyo vitano vitakuwa vituo vikuu na kusisitiza kuwa, marufuku kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kutumia pesa za Mfuko wa Barabara kulipana posho na kuacha kutengeneza barabara.
“Mkurugenzi wa TANROADS fuatilia fedha zote wanazopewa Wakurugenzi na kama watatumia vinginevyo, nipeni majina yao niyapeleke kwa Rais Jakaya Kikwete awafukuze kazi,” alisema.
Alitolea mfano wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato na Longido kuwa ndizo zimetumia vibaya fedha za mfuko wa barabara.
Ili kupunguza msongamano katika barabara ya Dar es Salaam hadi Chalinze mkoani Pwani, Dkt. Magufuli alisema itapanuliwa hivyo aliwataka wenye nyumba zilizopo katika Hifadhi ya Barabara zibomolewe vinginevyo atazivunja kwa kuwa yeye ndiye msimamizi wa TANROADS.
Alipiga marufuku barabarani kuwekwa matuta akisema sheria haziruhusu kwani magari yanaweza kuharibika wakaidai TANROADS.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TANROADS Bw. Patrik Mfugale, alisema kituo hicho kina uwezo wa kuingiza magari 80 kwa wakati mmoja na zaidi ya sh. bilioni moja zimetumika kufanikisha ujenzi wake.
SAFI SANA
ReplyDeleteHAKIKISHA ULIYOYAAGIZA YANATEKELEZWA KWA SABABU HAO WAMEZOEA KUSIKIA NA KUCHEKA KISHA WANAYAACHA HAPOHAPO!
ReplyDeleteFANYA KAZI YAKO BABA MAGUFURI,WANANCHI WAKO TUNA KUKUBALI VIBAYAMNO,KWA UTENDAJI WAKO USIO NA UBABAISHAJI.KAZA MWENDO!!!!!!!!!!
ReplyDeleteTangu agizo limetoka ni kweli hiyo bomoabomoa imekwishaanza au ndio mambo ya siasa tena!nijuzeni jamani kwani nipo mikoani huku.
ReplyDeleteMheshimiwa umechaguliwa na wananchi una kila hakiya kusikiliza waliokuchaguwa hivyo tunakuomba uwasimamiwe wavunjaji wavunje hata kama ni alama ya chama cha siasa kwani viongoziwetu wanpenda kujifanya wasanii wewe usikubali na hata Rais aliyekupa Uwaziri mheshimu kwa heshima yake ya urais kama ni mkunwa ako kiutawal lakini pale pale Rais anasign sheria inapotungwa lakini kuitimiza anogopa asikosa kula sio kura tumechoshwa na viongozi tunawpa mlo lakini sie hata kipapatiro wanashindwa kutupa Hongera.Mheshimiwa Magufuli.
ReplyDelete