*Kuivaa Kagera Sugar leo
Na Elizabeth Mayemba
BAADA ya kusonga mbele kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho (CAF) kwa kuichapa Kiyovu ya Rwanda mabao 2-1, Simba leo inashuka uwanjani kucheza na Kagera Sugar, katika mechi yao ya Ligi Kuu itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Simba inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 37 sawa na Yanga isipokuwa zimetofautiana idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Hivyo Wekundu wa Msimbazi Simba, leo wana kazi nzito ya kuhakikisha wanazoa pointi tatu, ili kuendelea kukaa kileleni.
Katika mzunguko wa kwanza timu hizo zilipokutana katika Uwanja wa Kaitaba, Bukoba Simba ilishinda kwa bao 1-0 hivyo itataka kuhakikisha inalinda heshima yake.
Akizungumzia mchezo wa leo Kocha Mkuu wa Simba Mserbia Milovan Cirkovic, alisema wamejipanga vizuri kuhakikisha wanaondoka na pointi tatu, ili waendelee kukaa kileleni.
"Tumejiandaa vya kutosha kuondoka na ushindi leo, hivyo nimewataka wachezaji wangu wawe makini wasiruhusu makosa ya kizembe, kwani tukifungwa tutakuwa tumejiweka pabaya kimsimamo," alisema Milovan.
Alisema kila timu imepania kuondoka na ushindi, hasa kipindi hiki cha lala salama, hivyo nao hawatabweteka hata kidogo.
Kocha huyo alisema leo atamkosa kiungo wake Haruna Moshi 'Boban', ambaye bado anatumikia kadi nyekundu.
Wakati Simba wakijigamba kuondoka na ushindi leo kwa upande wa Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Salum Mayanga ametamba kuwafunga wapinzani wao.
"Tumetoka Kagera kwa lengo moja tu la kuondoka na pointi tatu leo, hivyo Simba wasitarajie mteremko kutoka kwetu," alisema Mayanga.
Mechi nyingine itakayochezwa leo ni kati ya Azam FC na Coastal Union, itakayofanyikia katika Uwanja wa Azam Chamazi, Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment