08 March 2012

Jinsia izingatiwe kwa maendeleo ya jamii

LEO wanawake wa Tanzania wanaungana na wenzao duniani kote kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani inayoadhimishwa Machi 8 kila mwaka.

Maadhimisho ya mwaka huu Kitaifa yatafanyika Kitaifa mkoani Arusha na kauli mbiu "Ushiriki wa Wasichana Unachochea Maendeleo"

Lengo kubwa la siku hii ni kutoa fursa kwa makundi ya wanawake, jamii, vyama vya siasa,serikali na mashirika ya hiari kutafakari kwa makini matatizo mbalimbali yanayowakabili wanawake duniani kote.

Wanawake hutumia siku ya leo kuweka mikakati na kutafuta njia madhubuti ya kuleta ukombozi na maendeleo kwa wanawake ambao wamekuwa wakikandamizwa, kunyanyaswa na kudhalilishwa na jamii kutokana na mfumo dume ulioanzishwa enzi za mababu zetu na kudumu na kudumu kwa miaka mingi.

Pia kujenga mshikamano wa wanawake duniani kote na kutoa nafasi ya kuelimisha jamii kuhusu masuala mbalimbali ya wanawake pamoja na kuwahamasisha wanawake na jamii kwa ujumla kuhusu utekelezaji ahadi mbalimbali za serikali  zenye lengo la kudumisha amani, usawa na maendeleo.

Kwa kuwa wanawake wamekuwa wakinyimwa nafasi ya kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo jamii inatakiwa kubadilisha mtazamo na kuwashirikisha watu wa jinsia zote ili kuweka uwiano katika shughuli za kuboresha maendeleo ya jamii na afya ya jamii pamoja na kukuza uchumi wa Taifa.

Ili kuweka uwiano sawa, serikali na jamii inatakiwa kutoa kipaumbele katika elimu na siasa, kuwapa wanawake nafasi ya uongozi pamoja na fursa ya kutoa maoni ya kufanya maamuzi katika ngazi ya familia.

Wawanawake wanatakiwa kupata fursa ya kutoa maoni juu ya mpango wa uzazi na jinsi ya kuendeleza familia kwa kuwa wanawake ndio wanaobeba jukumu la kulea familia.

Pia wanawake wanatakiwa kupewa kipaumbele katika elimu kwa kuwa walibaguliwa na kunyimwa fursa ya kusoma jambo linalosababisha wanawake waonekane kuwa ni wajinga na wasio na uwezo.

Ili kuzingatia usawa, serikali inatakiwa kubadilisha mitaala ya elimu ili kuondoa mfumo dume wa kuweka mazingira yanayotoa fursa sawa kwa wote ikiwa ni pamoja na kuhamasisha jamii kutambua umuhimu wa kuwaendeleza wasichana sawa na wavulana.

Kwa ujumla jamii inatakiwa kuondokana na dhana potofu kuwa wanawake ni viumbe dhahifu ili kujenga mazingira yanayowashirikisha watu wote kwenye shughuli za maendeleo bila ubaguzi.

Wanawake wanatumia siku ya leo kuutangazia ulimwengu hususani Watanzania kuwa wana uwezo wa kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo pengine hata kuliko wanaume na wanachihitaji ni ushirikishwaji na fursa ya kufanya maamuzi.


No comments:

Post a Comment