02 March 2012

Askari polisi waundiwa tume

Na Mwajabu Kigaza, Kigoma
JESHI la Polisi mkoani Kigoma limeunda Tume kwa ajili ya kufanya uchunguzi juu ya tuhuma zinazowakabili baadhi ya askari polisi mkoani humo kuhusiana na usafirishaji haramu wa pembe za ndovu kwenda nchini jirani ya Burundi.


Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kigoma jana Kamanda wa Polisi mkoani humo, Bw.Fraisser Kashai alisema tume hiyo ya uchunguzi itaongozwa na Mkuu wa Upelelezi mkoani humo, Bw.Joseph Konyo nia ni kufanya uchunguzi wa kina kujua undani wa jambo hilo.

Alisema, kuundwa kwa tume hiyo kunafuatia habari zilizoandikwa na gazeti moja la kila siku (si Majira) likieleza kuwepo kwa askari polisi ambao walikuwa wakihusika na usafirishaji huo wa pembe za ndovu kwenda nchini jirani.

Kamanda huyo wa polisi mkoani humo alisema, sambamba na kuongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa mkoa pia tume hiyo itawajumuisha maofisa wengine kutoka, Idara ya Uhamiaji, Usalama wa Taifa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

Katika tukio lingine mwanafunzi mmoja wa Shule ya Sekondari Kagongo iliyopo Kigoma Vijijini amefariki dunia alipokuwa akiogelea eneo la Kibirizi kando kando ya Ziwa Tanganyika Mjini Kigoma.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Bw.Fraiser Kashai amemtaja mtoto huyo kuwa, Bw.Saidi Juma katika tukio lililotokea majira ya saa 2:00 usiku katika eneo hilo na kwamba mwili wake umepatikana na kukabidhi kwa ndugu zake kwa ajili ya mazishi baada ya kufanyiwa uchunguzi.

Bw.Kashai alitoa mwito kwa wazazi kuwa waangalifu na kutowaruhusu watoto wao kwenda kuogelea ziwani wakiwa peke yao kutoka na ziwa hilo kuwa na kina kirefu.

No comments:

Post a Comment