Na Patrick Mabula, Shinyanga
ZIARA ya Waziri Mkuu, Bw.Mizengo Pinda aliyoifanya hivi karibuni wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga imeacha manung’uniko kwa wanachi mbalimbali ambapo wananchi hao wanadai kukosekana kwa ratiba ya mkutano wa hadhara ni sababu moja wapo iliyowanyima haki ya kuonana naye ana kwa ana.
Wananchi hao walidai walikuwa na hamu ya kumuona na kuongea na Bw.Pinda ana kwa ana ili waweze kumueleza kero zao na changamoto zinazowakabili hususan sekta ya maendeleo.
Hata hivyo kwa mjibu wa ratiba ya ziara hiyo ya siku moja ambayo Bw. Pinda alifanya mjini humo hivi karibuni ambayo ilipangwa na Serikali wilayani Kahama ilionesha kutokuwepo kwa mkutano wa hadhara hali iliyofanya wananchi waliotaka Waziri Mkuu awahutubie kudai kunyimwa haki yao.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana kwa niaba ya wananchi wake Diwani wa Kata ya Kahama Mjini, Bw. Abas Omari alisema, baada watu kujua kuwa Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda atakuwa na ziara wilayani humo walimsubiri kwa hamu na kwa vile walikuwa na imani lazima angehutubia katika mkutano wa hadhara.
Alisema, wananchi hao walimsubiri kwa hamu kiongozi huyo wa Kitaifa na kujua atafanya nao mkutano wa hadhara na angetoa ufafanuzi wa kero na changamoto mbalimbali za maendeleo zinazowakabili na jinsi Serikali ilivyokusudia kuzishughulikia hatua baada ya hatua.
Kwa upande wake, Bw.Bobson Wambura ambaye ni Diwani wa Kata ya Majengo alisema, kitendo cha Serikali kuacha kumpangia mkutano wa hadhara wa Waziri Mkuu ili kuzungumza na wananchi katika Makao Makuu ya Wilaya ya Kahama kimewanyima fursa wananchi kumweleza kero na changamoto zilizopo.
Katibu wa Baraza la Wazee Wilaya ya Kahama, Bw.Paulo Ntelya alisema, walikuwa na matumaini na matarajio kuwa Waziri Mkuu, Bw.Pinda agekutana na baraza hilo lakini fursa hiyo waliikosa kutokana na ratiba ambayo ilipangwa hivyo wao kama wazee kukoseshwa haki yao ya kuwasilisha changamoto mbalimbali wanazoziona kwa lengo la kuharakisha maendeleo.
Bw.Ntelya alisema, kuna hoja ambazo walishaziwasilisha kwa Waziri Mkuu mjini Dodoma na kumpatia tangu Juni 15, 2011 ambapo baadhi ya hoja alizodai kwanini Halmashauri ya Mji wa Kahama ambayo ilishatangwaza kisheria na kupewa hati rasmi hajaanza kufanya kazi na pia hadi sasa imenyimwa hata fursa ya kukusanya mapato hivyo walitegemea ujio huo agewapatia majibu.
Aidha, alisema jambo jingine ambalo walishalipeleka kwake ni utendaji wa Halmashauri ya Kahama wamekuwa hawardishwi nao kutokana na kuwepo kwa kero nyingi moja ubovu wa barabara mbalimbali, migogoro ya ardhi na viwanja, umeme na pia walitaka kujua huduma za migodi ya dhahabu zinawanufaishaje kwa sababu hawaoni faida yake.
Naye Mzee Mashaka Kilonda ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Wilaya ya Kahama alisema, majibu ya hoja nyingine waliyotarajia kujua kwa faida ya wananchi ni kwa nini Wilaya ya Ushetu iliyokuwa imegawanywa toka Kahama ilifutwa wakati alikuwa ameitangaza kwa niaba ya Rais kwenye Bunge la mwaka 2010.
Hata hivyo hali ya kutokuwepo kwa mkutano wa hadhara kwa Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda ili kuzungumza na wananchi wa mjini humo kwenye ratiba ya ziara ya Waziri huyo imewaacha njia panda na kufanya kuwepo kwa manung’uniko katika mikusanyiko mbalimbali huku kila mmoja akidai kutotendewa haki.
Kwa mjibu wa ratiba iliyokuwa imetolewa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama awali na nakala yake kupewa waandishi wa habari ilieleza Waziri Mkuu akiwa Kahama ageweka jiwe la msingi katika Karakana ya Zana za Kilimo na kuwasalimia wananchi ambao wagekuwa wamefika hapo na kisha kuondoka.
Ndio ubabaishaji wa viongozi wanaodai kutuongoza kwani wanaficha maovu yao pindi wakiona wananchi watalalamika kwa viongzi wa juu,watambue siku zinakuja na ubabaishaji wa namna hii utakuwa historia.
ReplyDelete