Na Jovither Kaijage, Mwanza
WENYEVITI wa halmashauri za wilaya nchini wametakiwa kuendesha vikao kwa kufuata taratibu, kanuni na sheria ili kutoa fursa sawa kwa wajumbe wa vikao hivyo kutoa maoni yao.
Mwito huo ulitolewa jana katika mafunzo ya siku tatu ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza ambayo yanaendelea katika Mji wa Nansio.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Bw.Emanuel Omuyanja aliwaeleza madiwani hao wakati akiwasilisha mada ya kanuni za kudumu za halmashauri kuwa zipo taarifa za baadhi ya wenyeviti wa halmashauri na hata meya wa manispaa na jiji huwa wanazikiuka wakati wa kuongoza vikao.
Alisema, mbali ya tatizo hilo pia uchunguzi wake umebaini baadhi ya viongozi hao wa madiwani wanausika na vitendo vya upendeleo wakati wa vikao na hata wakati mwingine wanapanga wajumbe watakaotoa hoja katika vikao.
Bw.Omuyanja ambaye ni Ofisa Ushirika Mkoa wa Mwanza alisema, vitendo hivyo vikiendekezwa vinaweza kusababisha matatizo makubwa ikiwa ni pamoja na kukwamisha maendeleo na hata halmashauri husika kushindwa kujiendesha hivyo kufikia hatua ya kuvunjwa.
Alisema, baadhi ya halmashauri za wilaya katika Mkoa wa Mwanza zinakabiliwa na matatizo makubwa kama hayo na kuwa katika hatari ya kuvujwa baada ya kushindwa kusimamia majukumu yake.
Mmoja wa madiwani waliyeibua hoja hiyo, Bw.Gatawa Misana wa Kata ya Kagunguri kupitia Chadema alisema, ni vema ikatungwa kanuni ya kusimamia na kuzuia wenyeviti wa halmashauri wanaoweza kutumia nafasi hizo kwa maslahi binafsi hasa wakati wa kuongoza vikao.
Naye Diwani wa Kata ya Kakerege, Bw.Juma Mazigo (CCM) alisema, vitendo vya namna hiyo vikitokea hasa kubagua baadhi ya wajumbe kutoa maoni yao inaweza kuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo.
Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Dkt. Leonard Masale alisema, vitendo hivyo vinatokea katika baadhi ya halmashauri nchini, lakini ni hatari kwa maendeleo ya wananchi na pia ni chanzo cha vurugu na kutoelewa baina ya viongozi.
No comments:
Post a Comment