Na Salim Nyomolelo
KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC)imeishutumu serikali
kwa kushindwa kushindwa kutoa sh. bilioni 1.6 za kuwalipa wamiliki wa nyumba katika eneo la Mlonganzira Dar es Salaam ili kupisha ujenzi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Afya na Sayansi (MUHAS).
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam, mwenyekiti wa kamati hiyo Bw. Zitto Kabwe alisema, serikali imekopeshwa Dola za Marekani bilioni 74 zilizotolewa na Korea ya Kusini kwa lengo la ujenzi huo ili kuongeza idadi ya madaktari nchini.
Alisema, fidia ya sh. bilioni 8.06 tayari ilitolewa kwa wamiliki wa nyumba hizo na bado sh. bilioni 1.6 ili kumalizia fidia ya nyumba zilizobaki.
Alisema, cha kushangaza zaidi ni kwamba serikali ilitenga bajeti kwa mwaka 2009/2010, 2010/2011 na 2011/2012 lakini fedha hizo serikali imeshindwa kuzitoa.
Alisema kuwa, mradi wa ujenzi ilibidi kuanza Machi mwaka huu kutokana na mkataba uliosainiwa mwaka 2010.
"Kuna hatihati ya kuupoteza mradi huu kama fidia ya kuwalipa wamiliki hao haitatolewa na serikali jambo ambalo litasababisha kukosa hizo dola bilioni 74," alisema Bw. Zitto.
Alisema, kama chuo kikikamilika kinaweza kuzalisha madaktari 900 kwa kila mwaka wakati mahitaji ya madaktari kwa mpango wa maendeleo ifikapo mwaka 2015 ni 1,200 kwa mwaka.
Alisema takwimu zinaonesha kuwa, kwa sasa daktari mmoja anahudumia wagonjwa 50,000 huku baadhi ya mikoa kama Mara daktari mmoja anahudumia wagonjwa 100,000.
Alisema, wao kama kamati hawakubali fedha hizo zipotee huku nchi ikiwa na uhaba mkubwa wa madaktari, 'tumemuagiza katibu mkuu wa Wizara ya Fedha na Katibu mkuu wa Wizara ya Afya wafike ili watueleze msimamo wa serikali kuhusu suala hilo,' alisema.
Bw. Mukurtaza Mangungu mjumbe wa kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Kilwa Kasikazini alisema, anashangazwa na watendaji wa serikali na wakuu wa idara kukosa utaratibu wa kulipia miradi ya kuwasaidia wananchi.
Makamu mkuu wa chuo hicho Prof. Kisali Pallangyo alisema, tayari bilioni 8.06 zililipwa kwa jumla ya wakazi 1919 na wakazi 604 bado hawajalipwa fidia zao.
Alisema baada ya mradi kukamilika, chuo kitakuwa na uwezo wa kudaili wanafunzi 12,000 kwa mwaka wakati hivi sasa wanajumla ya wanafunzi 2000.
Waziri wa fedha Bw. Mustafa Mkulo alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu kushindwa kutoa fedha hizo kwa ajili ya kulipa fidia alisema, hana taarifa yoyote na kwamba, kama kuna bajeti hiyo itakuwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ama Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Bw. Ramadhani Khijjah alisema, kama kutakuwa na bajeti fedha hizo zitaweza kulipwa kabla ya muda huo kumalizika na kuongeza kuwa, hakuwa na taarifa hizo.
No comments:
Post a Comment