Na Rose Itono
TABIA ya madereva wa daladala kukatisha ruti imekuwa ikiwasumbua wananchi kwa kuwaongezea mzigo
kwa kulazimika kuunganisha usafiri pasipo na sababu.
Tabia hii imekuwa ikiendelea huku baadhi ya askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani wakiangalia hali hii bila kuwachukulia hatua za kisheria madereva wanaokiuka sheria za barabarani.
Hali imeonekana kuwa mbaya zaidi kwa wananchi wanaoishi katika maisha ya kawaida yaani wale wa kipato cha chini kwani wamekuwa wakijikuta wanalazimika kutembea kwa miguu kwa kushindwa kupanda mabasi mengine.
Hii yote ni kutokana na kukwepa gharama ambazo zimekuwa zikiongezeka kutokana na baadhi ya madereva kuwanyanyasa kwa kukatisha ruti bila sababu za msingi.
Maeneo yaliyoathirika zaidi na tatizo hili kwa jiji la Dar es Salaam ni mengi na si kwamba yapo pembezoni mwa mji la hasha.
Cha ajabu mijini ndipo vyombo vya dola vilipo huo ndio wajibu wa kikosi hicho cha usalama barabarani kulifumbua macho na kulishughulikia tatizo hili haraka iwezekanavyo.
Hali ya sasa ya maisha ni ngumu sana hivyo ifike wakati zile nyongeza za matumizi ambazo si za lazima ambazo wananchi wanaongezewa bila sababau ikiwa na kulazimishwa kuunganisha usafiri wa daladala kutokana na madereva kukatisha ruti zifanyiwe kazi haraka.
Kutolifanyia kazi tatizo hili kunaendelea kuwaumiza wananchi wengi wa kipato cha chini kwa kushindwa kumudu gharama hizo.
Ukweli ipo sababu ya kuliangalia tatizo la usafiri wa daladala hasa zile ambazo zimekuwa na kawaida ya kukatisha ruti na kuwasababishia wananchi kero.
Madereva wa daladala wamekuwa wakilifanya tatizo hilo kuwa gumu zaidi kwa wananchi wanaotumia vyombo hivyo kutokana na kutochukuliwa hatua zozote za kisheria pale wanapoamua kufanya mambo yao kinyume na taratibu.
Ili kukomesha hilo ni muhimu viongozi wakaonyesha mfano kwa kuwakamata madereva na kuwafikisha katika vyombo vya habari ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.
Nashangaa gari zinaandikwa sehemu inayotokea kwa mfano Kiwalani Mnazi mmoja lakini matokeo yake wanakatiza ruti yake kwa kuishia mtaa wa Kongo huku, askari wa kikosi cha usalama barabarani wakiangalia bila kuwachukulia hatua.
Nikiangalia kwa undani tatizo hili linatokana na jamii kubwa kutojua haki zao na kujikuta wakishuka kwenye basi bila kufikishwa katika kituo husika.
Ukweli hata madereva wanaofanya hivyo si kwamba hawajuhi kuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria bali wamekuwa wakitumia nafasi ya ufahamu mdogo wa wananachi kutojua haki zao kuwanyanyasa.
Sambamba na kutembea kwa muda mrefu kwa kushindwa kumudu gharama ya kuunganisha mabasi tatizo hili pia linachangia kuwafanya watu kuchelewa kufika katika majukumu yao ya kazi.
Mbali na kuchelewa pia wapo wanaojikuta wakipoteza vibarua vyao kutokana na kuchelewa hali ambayo inachangia kuongeza umasikini kwa taifa.
Serikali ilingilie suala hili kwa kuangalia tatizo la usafiri wa daladala ambazo zinakatisha ruti na kuwapa adhabu mbalimbali ikiwapo ya kuwafutia leseni.
Pamoja na eneo la Kiwalani kuwa linaongoza kwa mabasi yake kukatisha ruti na kuishia kituo cha mabasi cha Kongo badala ya kufika Mnazi mmoja yapo maeneo mengine ambayo yana tatizo kama hili.
Hali ni mbaya sana kwani daladala zote zikiwa na utaratibu wa kukatisha ruti jambo hili litasababisha usumbufu kwa wananchi.
Shughuli nyingi za kiuchumi pia haziwezi kufanyika kwa wakati kutokana na watu kuchelewa jambo linalochangia kuzozofidha uchumi wa nchi.
Asilimia kubwa ya watu wanaofika vituoni kusubiri usafiri wa daladala ili kuwahi shughuli zao za uzalishaji wanalazimika kusimama na kusubiri kwa muda mabasi ambayo yanaishia njiani na kugeuza.
Japo vikosi vya usalama barabarani vipo lakini ifike wakati tukubali kuwa vimepuuza kazi yao au kuzidiwa.
Utakubaliana na mimi kwamba bado Tanzania kuna tatizo pale inapotokea dharura kushindwa kuimudu kwa kuwa mamlaka husika zinazidiwa nguvu kutokana uzembe.
Naamini kabisa hakuna mtu yoyote ambaye anaweza kushindana na serikali iwapo serikali itaamua kikamilifu kufanya kitu kwa maslahi ya wananchi wote na taifa kwa ujumla.
Ieleweke wazi kwamba kwa kipindi kirefu sana madereva wa daladala wamekuwa wakinyanyasa abiria kwa kuwaishia njiani kutokana na kupata vichwa kutoka kwa watendaji ambao ni viongozi wa serikali.
Kitendo cha kukatisha ruti si jambo la kulaumu wananchi ambao hawaelewi kuwa wana haki za kugoma na kumlazimisha dereva amfikishe kituo husika.
Kiukweli haya yote hujitokeza mara jwa mara kwa kuwa si wananchi wote hasa wanaotumia usafiri wa daladala na hata madereva wenyewe na makondakta wanaelewa wanachotakiwa kukifanya kwa abiria wao.
Pia kuna haja ya serikali kutumia chombo husika kuwapatia elimu madereva wa daladala kuhusu sheria mbalimbali ikiwemo na ile kutoruhusiwa kukatisha ruti.
Hili nimelisema huenda hata madereva hawajui kama kufanya hiovyo ni kosa la kisheria na kubaki wakiona kuwa ni haki yao kufanya hivyo.
Kutokana na tabia hiyo ni jukumu la serikali kuhakikisha kwamba dharura zinapojitokeza zinashughulikiwa haraka iwezekanavyo pasipo kuleta madhara kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment