23 January 2012

Kuna tatizo la viongozi wasiowajibika

Na Peter Mwenda

SERIKALI inajitahidi kuondolea wananchi wake kero mbalimbali katika sekta
mbalimbaliikiwemo Afya, Elimu, Kilimo na Miundombinu.

Lakini watendaji wanaopewa majukumu ya kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo wamekuwa kikwazo hivyo kusababisha wananchi kulalamikia serikali yao kuwa haiwajali.

MBunge wa Jimbo la Kisarawe Bw. Selemani Jafo amekuwa akisimama kidete kushirikiana na wananchi wake kugomea miradi ambayo haijakamilika kulingana na mikataba ilivyofikiwa.

Bw. Jafo ambaye alichaguliwa kuwa mbunge katika Uchanguzi Mkuu Mwaka 2010 (CCM) anasema, udhibiti huo wa miradi ya maendeleo umefanikiwa kwa kiasi lakini bado kuna tatizo kubwa la uongozi usiowajibika katika vijiji vingi vya wilaya ya Kisarawe.

'Kuna watendaji katika sekta mbalimbali katika wilaya hii hawafanyi kazi bila kusukumwa, suala hili nitapambana nalo kuhakikisha kila mtumishi anawajibika, imefika wakati wanakisarawe wenyewe waungane kujenga wilaya yao" anasema Bw. Jafo.

Sekta ya maji

Mbunge Jafo anasema, wananchi wa Kisarawe ambayo wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji wameamua kupunguza matatizo ya maji kwa kuipokea miradi ya kuchimba visima na kusimamia kwa dhati.
Anasema, mradi wa kuchimba visima katika Wilaya ya Kisarawe ilikuwa inanze kutoka Oktoba mwaka jana kwa ufadhili wa mradi kutoka Benki ya Dunia ambako kimechimbwa kisima kirefu katika Kata ya Chole.
Awali anasema, kata hiyo dumu la maji lilikuwa likiuzwa sh. 1,500 kisimani kabla ya kubeba kupeleka nyumbani na maji hayo yalikuwa yakipatikana katika Kata ya Vikumburu ambako wananchi walitembea umali mrefu kuyafuata maji hayo.
Anasema, mpaka sasa vinachimbwa visima katika Kata za Msanga, Vikumburu, Kwala, Chole na Kihale ambavyo vikikamilika na kutoa maji ya kutosha Wilaya ya Kisarawe kwa asilimia 40 itakuwa imepunguza kero ya maji.
Bw. Jafo anasema, kisima cha Boga kilichopo Kata ya Maneromango ni moja ya mikakati ya vijiji vinne ambavyo vitachimbwa visima kwa ajili ya kusambaza katika vijiji vingine.
Kijiji cha Boga ni mfano wa kuigwa na wanakisarawe wengine kwa sababu wako mstari wa mbele kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi.

"Nashukuru kusikia mliwawagomea wachimba kisima ambao walikiuka makubaliano ya kuchimba mita 150 badala yake walichimba mita 100 tu mkiwambia hicho si kisima chenu'alisema Bw. Jafo.
Kilimo Kwanza
Anasema,jitihadazimefanyika kuhakikisha wananchi wanapata pembejeo za kilimo na matrekta ya kutosha kulima katika kipindi hiki cha mzimu wa kilimo ili kufikia malengo ya serikali kupitia Kilimo Kwanza.
Anasema, amepata malalamiko kutoka Kata ya Marui kuwa wanashindwa kupata matrekta ya kulima mashamba yao msimu huu wa mvua.
Bw. Jafo anasema, Katibu wa Umoja wa wakulima kutumia matrekta katika Kata ya Marui, Bi. Zaina Semlangwa alimwambia mbunge huyo kuwa kukosekana kwa matrekta hayo kumewarudisha nyuma ya kufikia malengo yao mwaka huu.
"Mbunge sisi wananchi wako tunakabiliwa na matatizo makubwa ya kukosa matrekta ya kulima, tumemwambia diwani wetu lakini hakuna juhudi inayofanyika ya kutuletea matrekta, tupo tayari kulipa fedha yoyote kwa ekari," anasema Bi. Semlangwa.
Katibu huyo aliendelea kulalamika kuwa, kuna trekta la mkazi mmoja wa kata hiyo ambalo uwezo wake wa kulima ekari zaidi ya sita kwa siku haupo wakati kuna ekari zaidi ya 300 za wananchi wa Kata ya Marui ambao wanahitaji kulimiwa mashamba yao.
Bi. Semlangwa anasema, trekta dogo (Power Piller) la kata hiyo halina uwezo wa kulima katika kipindi hiki ambacho mahitaji ya kilimo ni makubwa.
Diwani wa kata ya Marui, Bw. Mussa Dilonga alipoulizwa na mbunge sababu za kushindwa kuwatafutia wakulima matrekta ya kulima kuendana na kasi ya Kilimo Kwanza alijibu kuwa, wakulima hao wameshindwa kung'oa visiki hivyo kusababisha majembe ya matrekta hayo kumeguka.
Miundombinu
Mbunge Jafo anasema, bado kuna changamoto inayowapata wananchi wa Jimbo la Kisarawe ambayo ni ubovu wa barabara ya kutoka Kisarawe kwenda Vikumburu ni mbovu ambayo inahitaji kufanyiwa ukarabati.
Anasema,serikali imenwahidi kuwa barabara hiyo itajengwa na kuongeza kuwa barabara ya lami itajengwa kwa awamu kuanzia bajeti ijayo ya Serikali Kuu.
Huduma ya Afya
Bw. Jafo anasema, Sekta ya Afya inakabiliwa na changamoto mbalimbali za kutokuwa na zahanati katika baadhi ya kata na kukosekana kwa dawa za kutosha.
Jitahada zake zimefanikiwa kupatikana kwa gari la wagonjwa katika Hospitali ya Manerumango ambalo linasaidia kupeleka wagonjwa wanaozidiwa kwenda katika Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe.
Anasema kuwa, kuna jitihada za kuhakikisha kuwa kila kijiji kinakuwa na zahanati na kusambaza umeme wa sola ili kutunza madawa na kurahisisha upimaji wa magonjwa kama malaria na mengine.
Bw. Jafo anasema, katika kipindi hiki kutoka achaguliwe kuwa mbunge watumishi wa umma ambao hawakuwajibika wamechukuliwa hatua mbalimbali za kinidhamu akiwemo daktari wa Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe aliyehamishwa kituto na kushushwa cheo.
Anasema, katika jitihada zake za kupatikana kwa huduma za afya kutumia Mfuko wa Jimbo ambao hupewa mbunge amezitumia kujenga Zahanati ya Sofu ambayo itahudumia vijiji vinne ya jirani.
Wilaya ya Kisarawe ina mapambano makubwa ya kujikinga na magonjwa ya kuambukiza ukiwepo UKIMWI ambao unaelimishwa kila kijiji kutumia vikundi vya uhamasishaji na utoaji elimu ambavyo kuna wawakilishi watendaji katika kila Kata ya Wilaya ya Kisarawe.
Bw. Jafo anasema, vijana wameanzisha kampeni ya kuelimisha wananchi kujikinga na UKIMWI kwa kuanzia ni katika Kata saba Vikumburu, Kisarawe, Chole, Kibuta, Msanga, Msimbu na Mzenga ambako barabara kuu zinapita na kwenye magulio.
Sekta ya Elimu
Anasema, taaluma Wilaya ya Kisarawe imeanza kupanda baada ya kudorora kwa miaka mingi ambako wanafunzi waliokuwa wakifaulu maksi za daraja la kwanza na pili walikuwa wachache.
Ufaulu wa wanafunzi umeanza kupanda ambako wilaya hiyo imeshika nafasi ya tatu katika Mkoa wa Pwani na idadi ya wanafunzi wanaokwenda Shule za Bweni imeanza kupanda.
Anasema, wilaya hiyo inakabiliwa ongezeko la mimba kwa wanafunzi wa kike kutokana na kutokuwa na mabweni hivyo kutoa nafasi ya kupanga mitaani na kutumia nafasi hiyo kujiingiza kwenye anasa na ngono.
Pia kumekuwa na tatizo la uhaba wa walimu wa Shule za Msingi na Sekondari na kutolea mfano shule ya msingi Boga yenye watoto 502 lakini walimu waliopo ni watano hivyo kunawanyima fursa wanafunzi kusoma masomo yote.
Wananchi wa Kijiji cha Boga, Manerumango Wilaya ya Kisarawe, Pwani ni mfano wa kuigwa na wananchi wengine kwa kujikusanya na kuendesha harambee ya kuchangisha fedha za kujenga matundu ya vyoo vya Shule ya Msingi Boga, ambako zaidi ya sh. 400,000 zilichangwa.
Bw. Jafo anasema, harambee hiyo iliyojumuisha wananchi wa kijiji hicho na waliowahi kusoma shule hiyo waishio Dar es salaam na sehemunyingine  nchini.
Nishati ya umeme
Anasema, wilaya hiyo yenye vijiji 87 vilivyogawanywa katika Kata 15, lakini toka Tanganyika na sasa Tanzania Bara ipate uhuru mwaka 1961 ni vijiji vinne tu vyenye nishati ya umeme ambavyo vitatu kati ya hivyo vimepakana na Wilaya ya Kinondoni.
Anasema, vijiji hivyo ni Kiluvya A, Mloganzila, Kiluvya B, ambavyo vimepakana na wilaya ya Kinondoni na wilayani Kisarawe ambavyo vina umeme na vingine vyote bado viko gizani.
'Baadhi ya watu wanaona Kisarawe ni shamba la bibi,haiwezekani walipwe watu ambao hawahusiki na mradi wa umeme,hao tutawashughulikia' anasema Bw. Jafo.

No comments:

Post a Comment