Kocha Polisi afurahia ushindi
Na Speciroza Joseph
KOCHA wa Polisi Dodoma, Rashid Chama amefurahia matokeo ya ushindi katika mechi yake, dhidi ya JKT Ruvu na kupanga kuendeleza ushindi ili kuiweka timu hiyo katika nafasi nzuri.
Polisi Dodoma juzi ilipata ushindi wake wa ugenini kwa kuifunga JKT Ruvu bao 1-0 katika mechi ya Ligi Kuu iliyochezwa katika Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam ushindi ambao umeiongezea pointi tatu na kufikisha pointi 12, ikiwa imevuka nafasi moja kutoka 13 hadi 12.
Akizungumza mara baada kumalizika kwa mchezo huo, Chama alisema matokeo hayo yametokana na kujituma na jitihada za wachezaji wake kwa kujua majukumu yao.
“Kupata ushindi wa ugenini ni furaha kwangu hii imetokana na kila mchezaji kujua majukumu yake, nitahakikisha hali ya ushindi inaendelea katika mechi zote za ligi,” alisema Chama.
Aliongeza kuwa hana muda mrefu tangu aanze kukinoa kikosi hicho, hivyo atatumia muda uliobaki kuhakikisha timu hiyo inakaa katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Kocha huyo alisema wachezaji wote wapo katika hali nzuri kwa kuwa wamepata mazoezi ya kutosha na mbinu za kuhimili kumalizia mzunguko huu katika nafasi nzuri.
No comments:
Post a Comment