Mwandishi wetu
NYOTA imeanza kung’ara kwa mbunifu wa mavazi anayekuja juu kwa kasi nchini, Doreen Estazia na lebo yake ya Estado Bird baada ya kualikwa kuhudhuria mkutano wa kujadili masuala ya Uchumi duniani (World Economic Forum) utakaonza kesho mjini Devos –Klosters, Uswisi.
Doreen ambaye mwishoni mwa mwaka jana aliibuka na mavazi yaliyojulikana kwa jina la What’s Your Freedom (WYF?) kwa ajili ya kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara alisema amealikwa kama mjasiriamali katika masuala ya ubunifu wa mavazi na atakuwa chini ya Global Shapers.
Alisema hii ni faraja kubwa kwake, kwani kipaji chake ndicho kimempa nafasi hiyo na kuwa mbunifu wa kwanza nchini kushiriki katika mkutano huo mkubwa.
Alifafanua kuwa sekta ya ubunifu wa mavazi, inajulikana kimataifa kwani mbali ya kupromoti nchi nje ya mipaka pia ni vivutio vya utalii kwa upande wa mavazi.
“Nashukuru kupata nafasi hii na nitaiwakilisha vyema Tanzania, hii ni fursa pekee ya kujitangaza kimataifa na hasa ikizingatiwa kuwa nimeanza kujihusisha na masuala ya ubunifu mwaka mmoja uliopita,” alisema kabla ya kuondoka juzi usiku.
Alisema ameanza kupata mwanga wa mafanikio na lengo lake kubwa ni kufikia hatua ya juu kabisa katika masuala ya ubunifu wa mavazi na wala si viginevyo.
No comments:
Post a Comment