MALABO, Equatorial Guinea
KOCHA wa Libya, Marcos Paqueta amesema itakuwa vigumu kutosikitika baada ya kupoteza mechi kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Equatorial Guinea katika Kombe la Mataifa ya Afrika, Jumamosi.
Mchezaji Javier Balboa alifunga bao pekee kwa wenyeji huku ikiwa zimesalia dakika nne, ambapo aliwainua mashabiki wenyeji waliokuwa na hamu kubwa ya kushangilia huku Libya wakisikitika.
"Tulianza vizuri sana na walikuwa katika udhibiti wetu. Ghafla timu ilijisahau na kuachia mpira. Tulimiliki mpira kipindi cha pili na walifunga bao lao kwa shambulizi la kushitukiza," Paqueta aliiambia Cafonline.
"Sisi tulijua itakuja kuwa vigumu kucheza dhidi ya wenyeji na umati mkubwa ukiwa nyuma yao. Sio mwisho wa hadithi kuna mechi nyingine mbili zaidi mbele."
Kocha huyo kutoka Brazil alikiri kuhusu kupatwa na mshtuko kwa kupoteza mechi na kufanya safari yao ya kutaka kufuzu hatu ya mtoano kuwa ya mashaka.
"Kama unapoteza mechi ya ufunguzi, mara nyingi ni vigumu kwenda mbele. Hii ilikuwa ni mechi muhimu kwa ajili ya kufuzu kwa raundi ya pili," alisema.
Alisema watacheza kwa kujituma ili kushinda mechi nyingine zijazo licha kwamba kundi lao lina timu ngumu.
Libya katika mechi ijayo itapambana na Zambia kesho, na kisha itachuana na Senegal siku nne baadaye.
No comments:
Post a Comment