Na Goodluck Hongo
Katibu mkuu Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Stargomena Tax. amekanusha madai yaliyotolewa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa Tanzania haitaki kuwa na mtangamano kuhusu uharakishwaji wa uundwaji wa shirikisho la kisiasa la Afrika ya Mashariki
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana,Dkt. Tax alisema si kweli hata kidogo kwamba Tanzania haitaki kuwa na utengamano na jumuiya ya Afrika ya Mashariki na kwamba lawama hizi hazina msingi kwani nchi yetu inaamini jumuiya ina faida nyingi kuliko hasara
Alisema serikali imekuwa ikisisitiza kuwa mtangamano sharti uende hatua kwa hatua kama ilivyoainishwa katika mkataba wa uanzishwaji wa jumuiaya katika ibara ya 5 kifungu cha kwanza
Kwa msingi huo sharti kuimarisha na kutekeleza kikamilifu umoja wa forodha na soko la pamoja; na wakati huo huo kukamilisha majadiliano ya uanzishwaji wa umoja wa fedha.Hapa ndipo tutakapoweza kusema tuko tayari kujadiliana jinsi ya kuanzisha shirikisho la kisiasa
"Serikali yetu iko makini katika kutetea na kulinda maslahi ya wananchi wake na katika majadiliano yoyote ya mtangamano kama ambavyo nchi nyingine wanachama wa jumuiaya ya Afrika Mashariki wanavyolinda na kuteteta maslahi ya wananchi wake " alisema Dkt Tax.
Akizungumzia uhuru wa raia wa shirikisho la Afrika Mashariki kufanya kazi katika nchi nyingine alisema ibara ya kumi ya itifaki ya soko la pamoja inawahakikishia raia wa nchi wanachama kupata ajira katika nchi yoyote mwananchama.
Dkt Tax alizitaja baadhi ya fursa zitakazo patikana kuwa pamoja na walimu wa vyuo vya elimu ya juu, vyuo vikuu wenye shahada ya uzamivu kuanzia mwaka 2010,walimu wa shule za sekondari katika fani ya hisabati,fuzikia,baiolojia,walimu wa lugha za kigeni,walimu wa vyuo vya kilimo,ufundi stadi wenye kiwango cha elimu ya shahada ya pili katika fani husika.
Fursa zingine ni wahandisi wa madini,majengo,maafisa ugani katika sekta ya kilimo,wauguzi na wakunga ,kada ya waongoza ndege na kada ya upimaji ramani na kuwataka watanzania kuacha hofu juu ya shirikisho hilo kwa kuwa hata watanzania wengine wanafanyakazi katika nchi hizo za jumuiya kwa kufuata vigezo na masharti ya nchi husika na fursa zote hizi zimezingatia kuwa sekta hizo zinaupungufu wa wataalamu hao.
Akizungumzia uazishwaji wa sarafu moja ya Jumuiaya hiyo alisema mchakato wa ukusanyaji maoni unaendelea na zoezi hilo linaangaliwa kwa upana wake siyo kukurupuka katika kufanya maamuzi.
Alisema kuwa inapofikia hatua hiyo lazima pawepo na usawa katika nyanja ya uchumi , viwango vya kubadilisha fedha za kigeni, na baada ya kukamilika kwa hayo ndiyo nchi wananchama wanaweza kufikia maamuzi ya kuazisha sarafu ya pamoja.
No comments:
Post a Comment