Na Mwali Ibrahim
CHAMA cha mchezo wa Judo Tanzania (JATA) leo kinatarajia kupanga tarehe mpya ya uchaguzi mkuu wa chama hicho katika kikao cha pamoja na Baraza la Michezo Tanzania (BMT)
JATA walishindwa kupanga tarehe rasmi ya uchaguzi tangu ile ya awali kuahirishwa kutoka na kuwa na muamko mdogo wa wagombea wanaojitokeza kuwania uchaguzi huo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa JATA, Kashinde Shabani alisema, sambamba na kuapanga tarehe hiyo pia watatumia kikao hicho kufikisha maadhimio ya kamati ya utendaji wa JATA wa kupunguza baadhi ya kamati za chama hicho kuonekana hazina tija.
Alizitaja kamati hizo kuwa ni kamati ya watu wa kujitolea ambayo wameifuta ikiwa ni pamoja na kamati ya ufundi ambayo imeunganishwa na kamati ya waamuzi ambayo itakuwa ni kamati moja katika nafasi za uongozi.
"BMT ndio wasimamizi wetu hivyo mabadiliko haya ni lazima tuwafikishie ikiwa ni pamoja na kushirikiana nao katika kupanga tarehe mpya ya uchaguzi," alisema Kashinde.
Alisema, lengo la hayo yote ni kutaka kuhakikisha chama kinakuwa na mabadiliko makubwa na kuweza kuwa ni moja ya vyama vyenye maendeleo makubwa kimichezo na hata kiuongozi hapa nchini.
No comments:
Post a Comment