Na Queen Lema, Arumeru
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha, Bw Anthony Musani, amewataka viongozi wa Jumuiya ya
Wazazi ya chama hicho wilayani humo, kuacha tabia ya kung'ang'ania madaraka.
Bw. Musani aliyasema hayo juzi wilayani humo wakati akizungumza na wajumbe wa jumuiya hiyo na kuongeza kuwa, umefika wakati wa viongozi hao kuachia nafasi zao kwa vijana ili kuimarisha demokrasia.
Alisema ndani ya umoja huo kuna baadhi ya viongozi ambao hawajui maana ya demokrasia ndio maana hawataki kutoka madarakani na kusababisha vijana kukosa haki zao za msingi.
Aliongeza kuwa, viongozi wanapaswa kuwa na uzalendo pamoja na kulinda heshma zao kwa kujivua gamba inapohitajika kufanya hivyo ili kukijenga chama hicho na kutoa nafasi kwa vijana ili kushika nafasi za uongozi na kuimarisha chama.
“Tusiruhusu demokrasia ibaki mikononi mwa baadhi ya watu na kuwaacha vijana wetu wakikosa nafasi za uongozi, kila kiongozi anapaswa kujua na kutambua anapaswa kutawala kwa muda mfupi na kuwaachia wengine badala ya kushikilia nafasi aliyonayo hadi mwisho wa uhai wake, tusifanye hivyo,” alisema.
Aliongeza kuwa, wananachi na wanachama wa CCM, wanapaswa kuweka utaratibu wa kumchagua kiongozi ambaye atawafaa na kutumikia jamii husika kwa kikomo ili kuondoa tofauti mbalimbali zinazojitokeza kwa sasa.
Alisema wanachama wa CCM wilayani humo, hawapaswi kumchagua kiongozi ambaye ni tajiri wa mali na fedha ili kuepusha madhara mbalimbali yanyoweza kutokea kwa chama hicho na jumuiya hiyo.
“Nawaomba wananchi wa Wilaya hii mkumbuke kuwa, rushwa ni adui wa haki, kamwe msikubali kuchagua kiongozi kwa kumuangalia, mnatakiwa kutumia demokrasia halisi.
“Kuna baadhi ya watu wanaotaaka kushika nafasi mbalimbali za uongozi katika chama au jumuiya kwa kutumia kigezo cha fedha au utajiri alionao hali ambayo inawafanya vijana wengi wakose haki ya msingi ya kuwa viongozi,” alisema Bw. Musani.
Aliwataka viongozi wote kuhakikisha wanakubaliana na
mabadiliko mbalimbali yanayotokea katika chama hicho.
No comments:
Post a Comment