30 December 2011

EAC yaibua miradi 244 sekta ya uchukuzi,nishati

Na Gabriel Moses

JUMUIA ya Afrika Mashariki (EAC) imekamilisha na kupitisha mkakati wa ushirikiano katika sekta ya miundombinu ya kiuchumi hususan miundombinu ya Uchukuzi na
Nishati.

Kutokana na hali hiyo jumla ya miradi 244 imeibuliwa kwa nchi wanachama na zinatarajiwa kuanza kutekelezwa mwezi Januari, mwakani.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Bartholomeo Rufunjo, alisema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi.

Dkt. Rufunjo ambaye alikuwa akizungumzia uendelezaji wa sekta ya miundombinu ya kiuchumi iliyofikiwa na jumuia hiyo hadi sasa alisema hatu hiyo itawezesha nchi wanachama kupiga hatua zaidi.

Alisema ujenzi wa miundombinu wa reli ya kati unatarajia kuanza mwakani na kuunganisha mikoa ya Tanga, Arusha na Mara.

Alisema ujenzi wa barabara ya Arusha kwenda Namanga pia unatarajiwa kukamilika mwezi Januari mwakani.

Alisema Tanzania katika mkakati huo imelenga kuziunganisha nchi za jumuia ya Afrika Mashariki na bandari za mwambao wa bahari ya Hindi ili kurahisha upatikanaji huduma muhimu zitumiazo bahari.

Dkt. Rufunjo alisema katika mkutano wao uliofanyika mjini Arusha na Mombasa nchini Kenya, Baraza la Mawaziri la sekta ya Uchukuzi, Mawasiliano na Hali ya Hewa (TCM), lilipokea taarifa za utekelezaji wa baadhi ya miradi na program mbalimbali katika sekta hizo

Alisema miradi 244 inazijumuisha nchi zote tano za Jumuiya na kwamba kila nchi itakuwa na mikakati yake katika kuunganisha nguvu za jumuia hiyo.

Kwa upande wa Tanzania alisema imeweka mkakati wa kuziunganisha nchi wanachama kwa kujenga miundombinu ya reli, barabara, usafiri wa majini na bandari, sekta ya nishati na utabiri wa hali ya hewa.

Kwa mujibu wa Dkt. Rufunjo, sehemu kubwa ya miradi iliyoko nchini imeanza kutekelezwa kwa kasi.

Alisema baadhi ya miradi inasubiri sekretarieti ya Jumuia hiyo kwa kushirikiana na nchi wanachana na Washirika wa Maendeleo kuanza mchakato wa kupanga jinsi ya  utekelezaji kutoka katika mkakati huo.

"Kukamilika pia kwa miradi hiyo kutategemea sana kuwapo kwa bajeti itakayokidhi matakwa, ipo mingine inaweza isitekelezwe kutokana na ufinyu wa bajeti ila mambo yakienda sawa kila jambo litakuwa sawa," alisema.


No comments:

Post a Comment