30 December 2011

EWURA yacharuka

*Bodi yafungia vituo vinne vya mafuta Dar
*Vilikaidi agizo la kujieleza kwa maandishi
*Kingine chapewa kusudio kusitishwa leseni
*DPP aombwa kufungua kesi uhujumu uchumi

Na Salim Nyomolelo

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), jana imeanza kuchukulia hatua ya kuvifungia vituo vinne vya mafuta Jijini Dar es Salaam ambavyo
vilifanya mgomo baridi wa kutouza bidhaa hiyo Desemba 19 mwaka huu.

Akizungumza na Majira Dar es Salaam jana, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano cha EWURA, Bw. Titus Kaguo, alisema uamuzi wa kuvifungia vituo hivyo umetolewa na Bodi ya Wakurugenzi ya mamlaka hiyo.

Alivitaja vituo hivyo kuwa ni GBP kilichopo Sinza, ambacho kilikataa kupokea oda ya agizo la kujieleza kwanini kisichukuliwe hatua kwa kugoma kuuza mafuta.

Kituo kingine ni Camel Oil kilichopo Veternary, Camel Oil (Tabata), na Gapco kilichopo Mbagala Rangi Tatu, ambavyo pamoja na kupelekewa oda ya kujieleza, vilishindwa kupeleka utetezi wao katika ofisi za mamlaka hiyo.

Bw. Kaguo alisema, kituo cha Mwenge Filing Station, kimepewa kusudio la kusitishiwa leseni ya kufanya biashara hiyo lakini kama mmiliki wake atakuwa na maelezo yanayojitosheleza, kitaruhusiwa kuendelea na biashara hiyo.

Aliongeza kuwa, kituo kingine ni Camel Oil Petro Station kilichopo, Ngarenaro mkoani Arusha ambacho Bodi imeagiza kifungiwe mara moja na kutoa maelezo ndani ya siku saba kwa sababu mmiliki wake alikataa kuuza mafuta ambayo yalikuwepo kituoni.

“Bodi ya Wakurugenzi pia imeshauri Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Eliezer Feleshi, amfungulie kesi ya uhujumu uchumi mmiliki wa kituo,” alisema.

Alisema uamuzi huo, ulifikiwa baada ya ukaguzi uliofanywa na EWURA kutokana na malalamiko ya wananchi na kugundua baadhi ya vituo vilikuwa haviuzi mafuta.

Akizungumzia uhaba wa mafuta uliopo katika mikoa ya Kilimanjaro, Mbeya, Sumbawanga na Kigoma, Bw. Kaguo alisema hali hiyo imetokana na mgomo baridi uliofanywa na wauza mafuta Jijini Dar es Salaam, Desemba 19 mwaka huu, ambao uliaribu mfumo mzima, kunyesha kwa mvua na kusababisha maeneo ya Mlima Kitonga kutopitika kwa upande wa kusini.

Alisema wakaguzi watakwenda kukagua hali ya upatikanaji wa bidhaa hiyo katika mikoa ya Kanda za Kaskazini (Tanga, Arusha na Moshi), Kanda ya Kusini na Kanda ya Ziwa.

4 comments:

  1. Inapendeza sana kuona EWURA sasa wameamua kutoa makucha yao. Safi sana!!!!

    ReplyDelete
  2. Masebu endelea na msimamo huo huo .hongera baba

    ReplyDelete
  3. Kwakweli,

    Wbsite yenu haieleweki. Sielewi wale ambao hawana knowledge ya IT kama wanaweza ku interested kuendelea angalau kuchungulia mnachoandika. Hebu jaribuni ku-update taarifa zenu. Inaboa kwa gazeti kubwa na kongwe kama majira kuwa na utendaji wa aina hii.
    Badilikeni

    ReplyDelete