30 December 2011

Wataka Katiba Mpya iondoe kinga kwa rais

Na Yusuph Mussa, Korogwe

BAADHI ya wananchi katika Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga, wamesema kama Katiba Mpya itaendelea kumlinda rais asishtakiwe akiwa madarakani na baada ya
kumaliza utumishi wake serikalini, upo uwezekano wa kutokea kiongozi ambaye atatumia fursa hiyo kufanya maamuzi yanayoweza kusababisha machafuko nchini.

Wananchi hao walishauri hoja ya mgombea binafsi ni vyema ikaruhusiwa ili kuwalinda viongozi wanaochaguliwa na wananchi ambao vyama vyao vinatishia kuwavua uanachama na kupoteza nafasi zao kutokana na migondano inayotokea ndani ya chama.

Wakazi hao waliyasema hayo juzi mjini Korogwe, katika mdahalo wa kujadili katiba iliyopo, kasoro zake na kutoa maoni yao ambayo wangependa yaingizwe katika Katiba Mpya.

Walisema umefika wakati wa rais kushtakiwa kama itabainika ameshindwa kuwajibika kwa kuhudumia wananchi wake.

“Kinga ya rais iondolewe kama itabainika amefanya makosa ili aweze kuwajibika kwa wananchi na kuifanya Ikulu yetu kuwa sehemu takatifu.

“Enzi ya uhai wake, Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema kuwa, Ikulu si mahali pa mchezo lakini katiba iliyopo inamlinda rais asiwajibishwe hata aanapofanya kosa,” alisema Bw. Renatus Mchau.

Naye Bw. Omar Chagogwe, alisema udikteta ulioingia katika vyama vya siasa dhidi ya viongozi waliochaguliwa na wananchi, hauwezi kukoma kama suala la mgombea binafsi halitaingizwa kwenye Katiba Mpya.

“Mgombea binafsi ni jambo la msingi sana kwani katika vyama vya siasa kuna fitina nyingi zinazowafanya wawakilishi wa wananchi washindwe kufanya kazi zao ipasavyo, kama mwanachama hawezi majungu, hawezi kupitishwa na chama chake kugombea uongozi.

“Kama tutakuwa na mgombea binafsi ambaye anakubalika na wananchi, watamchagua ili awatumikie, tunaomba Katiba Mpya izingatia jambo hili,” alisema Bw. Chagogwe.

Kwa upande wake, Mchumi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Bw. Lameck Kajala, alisema kitendo cha serikali kuteua wabunge kuwa mawaziri, kinapunguza uwajibikaji hivyo Katiba Mpya ione umuhimu wa kutenganisha mfumo huo.

Mchumi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe Bi. Grace Mbarouk, alisema Serikali imegawa madaraka kwa wananchi kinadharia lakini bado haizisaidii halmashauri kujiendesha kwani bado inachukua kodi zote na kuzipeleka Serikali Kuu.

Mshiriki mwingine katika mdahalo huo, Bw. Abdillah Ibrahim, alisema wakuu wa mikoa na wilaya wanapochaguliwa na rais ni vyema wakapigiwa kura, kuthibitishwa na wabunge kama ilivyo kwa Waziri Mkuu ili kuondoa watendaji wasio na sifa.

Akitoa mada katika mdahalo huo, Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Handeni, Bw. Jonathan Mgongoro, alisema Azimio la Arusha bado halijafa bali limeboreshwa ili kuwafanya watumishi wa Serikali wasipate shida baaada ya kustaafu na kuwawezesha wafanyabiashara kujiunga na siasa.

Muongozaji wa mdahalo huo na mjumbe wa Kamati ya Jukwaa la Katiba nchini, Bw. Esrael Ilunde, alisema kuna mipaka kwa wananchi kutoa maoni yao juu ya Katiba Mpya na wale ambao watavuka mipaka hiyo watashtakiwa na kufungwa jela.

“Ukifika wakati wa Tume ya Rais kukusanya maoni ya wananchi, alafu mtu akajifanya ni mjumbe wa tume hiyo au kufanya kosa lolote, atalipa faini kati ya sh. milioni tano hadi 15, kwenda jela miaka mitatu hadi saba au vyote kwa pamoja,” alisema.

Mwenyekiti wa Mtandao wa Asasi za Kiraia wilayani Korogwe (KOCISCO), ambao ndio waratibu wa mdahalo huo, Mchungaji Hebert Mwaimu, alisema lengo la mdahalo huo ni kuwaandaa wananchi kujua Katiba ya sasa na kujiandaa kuipokea tume hiyo.


6 comments:

  1. tunahitaji katiba tatu , ya wazanzibari , ya watanganyika na ya muungano, ya wazanzibari itachangiwa na wazanzibari , ya watanganyika itachangiwa na watanganyika na ya muungano itachangiwa na wote. Katiba mama yaani ya watanganyika au wazanzibari itakuwa na nguvu zaidi kuliko ya muungano itapotokea utata kutegemea na tatizo lilipo , ikiwa tatizo linahusu tanganyika katiba ya tanganyika itakuwa na nguvu kuliko yamuungano , vivyo hivyo iwapo tatizo linahusu zanzibar , katiba ya zanzibar itakuwa na nguvu kuliko ya muungano , huu ndio utaratibu tunaoutaka, ambao utahakikisha usawa na haki kwa wananchi wa pande zote. Wazanzibari wanataka wizara yao ya fedha, ya ndani , ya ulinzi , jeshi na polisi , mahakama na sheria , haya mambo yote yasiingizwe kwenye muungano. Tunataka tuachiwe visiwa vyetu tujitawale na tujiendeleze , na watanganyika waachiwe wajiendeleze wenyewe , tukae pamoja tuangalie mambo gani tunataka tushirikiane ktk muungano kwa faida ya pande zote, nimefikisha , wananchi wote wa zanzibar na tanganyika amkeni msilale , viongozi wa znz mnaokula rushwa hamjali maslahi ya waznz mkumbuke kuna siku mtakufa na kufika mbele ya Mungu kujibu dhuluma mlizowafanyia raia, hakuna atayeishi maisha , Karume katangulia , kafuatiwa na Nyerere kila mmoja atafika mbele ya haki,

    ReplyDelete
  2. Huo ndio ukweli, katiba tatu zinafaa zaidi pia kuepuka kuonekana wengine wanaonewa. Pia kinga ya Rais kutoshitakiwa ndiyo inayoleta kutowajibika kwa viongozi wengi na hakuna wa kuwawajibisha viongozi wabovu. Mfano tu, akina Ndugai kujibizana na waziri mkuu mstaafu, hii ni kuonyesha jinsi ambavyo hakuna anayeogopwa kapisa!!!!

    ReplyDelete
  3. mimi nawaunga mkono wote wanaozungumzia katiba tatu , serikali mbili ya Tanganyika na ya Zanzibar , na kuwepo na shirikisho kwa mambo tutayokubaliana kwenye muungano, kusiwepo serikali ya muungano ni gharama na mzigo kwa walalahoi, kila mtu abebe mzigo wake mwenyewe.

    ReplyDelete
  4. Na pia DPP Lazima achaguliwe na wananchi,na sio rais.kwani tuna taka hasimwogope rais wala ,waziri fulani,bali hawaogope wananchi waliomchagua.

    ReplyDelete
  5. Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ,hasichaguliwe na rais pia.achaguliwe na na taasisi [NGOS]

    ReplyDelete
  6. Katiba moja serikali moja au katiba tatu serkali tatu hakuna jingine.muundo wa sasa noma haufai kabisa viongozi ni wababaishaji mno

    ReplyDelete