18 October 2011

Zitto Kabwe, Makamba moto kwenye mdahalo

*Waibua kashfa matumizi mabaya serikalini
*Wataka waliojiuzulu Richmond walipe Dowans


Na Tumaini Makene

WAKATI makali ya mgawo wa umeme yakionekana kupungua huku nchi ikiwa bado katika hali ya udharura bila kupata suluhisho la kudumu, serikali imeingia
katika kashfa nyingine kubwa kufuja fedha za umma kwa uzembe wa watawala.

Kashfa hiyo inatokana na serikali kutumia mamilioni ya fedha za walipa kodi kuzalisha umeme wa dharura wa mafuta badala ya kutumia utajiri wa vyanzo vingine mbadala uliopo nchini kama gesi na makaa ya mawe kuzalisha umeme wa kudumu.

Kwa mujibu wa wataalamu, makaa yalipo nchini yanaweza kutunika kuzalisha umeme wa uhakika kwa miaka 150 ijayo, na madini ndiyo yaliyotoa mchango mkubwa kwa mapinduzi na maendeleo ya viwanda kwa nchi takriban zote zilizoendelea kuanzia Uingereza katika karne ya 18.

Taarifa za kitaalamu zinaonyesha kuwa uniti moja ya umeme unaozalishwa kwa mafuta unagharimu takriban senti 40-45 za dola ya Marekani wakati ule wa makaa ya mawe kwa kiwango hicho hicho inagharimu senti 10-12, huku ule wa gesi asilia ukigharimu kati ya senti 8-10.

Rasilimali hizo zote za asili pamoja na chanzo kingine cha nguvu ya upepo zinapatikana kwa wingi nchini, lakini kumekuwa na kigugumizi cha kutumika huku serikali ikitoa maelezo mengi kila mwaka kuhusu matumizi ya madini hayo, hivyo kuleta mawazo kuwa uenda watendaji wanapata asilimia 10 katika mikataba ya mitambo ya mafuta.

Wakizungumza katika mdahalo wa 'Nishati na Tanzania Tunayoitaka' juzi usiku, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw. Kabwe Zitto (CHADEMA) na Mbunge wa Bumbuli, Bw. Januari Makamba (CCM), walisema baada ya taifa kujisahau na kuchelewa kufikiria vyanzo mbadala tofauti na umeme wa maji, nchi imeingia katika kashfa nyingine ya ufujaji fedha za umma.

Mdahalo huo ambao Wizara ya Nishati na Madini ilitafsiriwa kuukwepa kwa kile kinachoaminika kuwa ni kukosa hoja za kujibu, ingawa awali ilidaiwa kuthibitisha kushiriki, ulivuta hisia za Watanzania wengi kwa kuuliza maswali mengi.

Wabunge hao walieleza washiriki wa mdahalo huo kuwa kukosekana kwa nishati ya umeme ni sawa na kuua injini ya kuendeshea uchumi, hivyo kuathiri ukuaji wa uchumi mkubwa na ule mdogo ambao unagusa maisha ya kila ya mwananchi wa kawaida.

Vyanzo vya umeme

"Kwa kweli hilo swali lako ndiyo swali langu pia nimekuwa nikijiuliza muda mrefu, nafikiri kama umenisikia hata bungeni nimekuwa nikiuliza mara kwa mara kwa nini mipango yetu ya umeme inaendelea kutegemea maji zaidi,...na tumekuwa tukisema hapa nchini kuwa tuhimize kilimo cha umwagiliaji kwa sababu mvua haziaminiki.

"Sasa kama mvua haziaminiki katika kilimo inakuwaje ziaminike katika kuzalisha umeme, mimi ninachosema tumechelewa sana, tumechelewa kufikiria njia mbadala na vyanzo vingine vya umeme, mfano matumizi ya makaa ya mawe katika kuzalisha umeme,...umeme wa makaa ya mawe ndiyo ulisababisha mapinduzi ya viwanda katika nchi zilizoendelea," alisema Bw. Makamba na kuongeza.

"Ni scandal (kashfa) kutumia fedha za kigeni kuzalisha umeme wa mafuta kama vile diseli na mafuta ya ndege ambao ni ghali sana wakati kuna vyanzo vingine vingi tu kama hayo makaa ya mawe, tumechelewa lakini sasa tuharakishe,...pia TANESCO igawanywe sehemu tatu, kuwepo TANESCO Uzalishaji, TANESCO Usambazaji na TANESCO Uuzaji," alisema.

Bw. Makamba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, alisema ili nchi iondokane na tatizo la nishati ya umeme ambalo limekuwa sugu kwa muda mrefu tangu mwaka 1992 ni muhimu kushughulikia matatizo ya mitambo ili kuzuia upotevu mkubwa wa umeme njiani.

Zitto na Richmond

Kwa upande wake, Bw. Zitto alienda mbali zaidi na kuweka wazi msimamo wake kuhusu malipo ya tuzo kwa Kampuni ya Dowans kwa kueleza kuwa kabla ya kulipwa wanasiasa waliowajibika kwa uzembe huo pamoja na watendaji walipe deni hilo kwanza.

Alisema mkataba huo ambao ni wa Richmond uliingiwa kimakosa na hata baada ya kuvunjwa kwake bado makosa yaliendelezwa hivyo kabla ya Watanzania kubebeshwa mzigo wahusika wawajibike kikamilifu kuilipa si kwa upande mmoja pekee.

Aliwataka Watanzania kuanzia wananchi wa kawaida hadi viongozi kuacha tabia ya kulalamika na kuwa mabingwa wa kuainisha matatizo badala yake wajielekeze katika kutoa masuluhisho ya matatizo yanayoikabili nchi.

Mbunge huyo alisema wakati yakifikiriwa mageuzi ndani ya TANESCO pia inapaswa kufikiriwa ni namna gani nchi inaweza kujilinda dhidi ya wawekezaji 'uchwara', ili kuepuka kuitumbukiza nchi katika masuala ya kashfa na mabishano kama yale ya Richmond na baadaye Dowans.

Alisema mikataba hiyo mibovu ndio iliyofikisha nchi hapa lilipo katika mtanziko na sintofahamu juu ya nishati ya umeme, hivyo ni lazima hatu za makusudi zichukuliwe mapema kukwepa hali hiyo siku zijazo.

"Tunaifikiaje dhamira ya kuongeza idadi ya wananchi wanaopata umeme, kutoka asilimia 14 ya sasa mpaka kufikia asilimia 30 ifikapo mwaka 2015,...kama ilivyoelezwa katika ilani ya CCM na CHADEMA, ...sina hakika sana CUF walisema nini, lakini mojawapo ni kuhakikisha tunakuwa na massive rural electrification (usambazaji mkubwa wa umeme vijijini).

4 comments:

  1. HAWA WOTE WANAFIKI TU HAWANA MAANA HATA SIKU MOJA, MBONA KIKWETE NI RAIS HUWA ANAONGEA KAMA WAO TU KUNATOFAUTI KWELI HAPO? ZITTO PANDIKIZI LA KIKWETE, JANUARY MAKAMBA ANATAKA UMAARUFU MAANA UCHAFU WA NISHATI UMEUCHANGIA SANA

    ReplyDelete
  2. Mnafikiria umeme wakati mnashindwa kuua hata mbu. Acheni porojo. Nchi kwisha kabisa. Hatua ya kwanza tufukuze Wahindi. Hakuna kashfa ambbayo brain ni mhindi

    ReplyDelete
  3. hakuna kashfa mhindi hayuko ndani

    ReplyDelete
  4. SAFI SANA WADAU DOWANSI ROSTAM AZZIZ/EPA JITTU PATEL/RADA VITALLAN SOMAIYA,HIVI NYINYI WANAWA TANZANIA WAHINDI NI NDUGU ZETU ILA WANATUTUMIA VIBAYA KUTUIBIA RASILIMALI ZETU KAMA WANATAKA UZALENDO TUWAPE MASHAMBA NA VIWANJA NJE YA MIJI WAYAENDELEZE SIO KUKAA KWENYE MAJUMBA YA MSAJILI WAKIWA NAUTAJILI WA KUPINDUKIA USIO SAIDIA KUSISIMUA UCHUMI ZAIDI YA KUUNYONYA MUNGU IBARIKI TANZANIA

    ReplyDelete