Na Zahoro Mlanzi
TIMU za Simba, Yanga na Azam FC katika michezo yao ya mwisho ya Ligi Kuu Bara, zimeingiza sh. milioni 85. Mapato hayo
yametokana na jumla ya fedha zilizopatikana katika mechi zao ambapo Yanga, ilicheza na Kagera Sugar na kuingiza sh. 42,810,000, Simba iliumana na African Lyon ambazo ziliingiza sh. 41,800,000 na Azam ilicheza na JKT Ruvu na kuingiza 909,000.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema mechi ya Yanga iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam iliingiza sh. 42,810,000 kutokana na watazamaji 11,559 waliokata tiketi.
"Kwa upande wa Simba watazamaji 11,787 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo ya Simba iliyochezwa Oktoba 16, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuingiza sh. 41,800,000," alisema Wambura.
Alisema mechi ya Azam iliyochezwa Oktoba 15, mwaka huu kwenye Uwanja wa Chamazi iliingiza sh. 909,000 kutokana na watazamaji 303 waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo.
Wakati huohuo, Ligi Daraja la Kwanza hatua ya makundi inayochezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini, inaendelea leo kwa mechi saba katika viwanja tofauti.
No comments:
Post a Comment