13 October 2011

Wafuata huduma ya maji nchini Kenya

Na Gift Mongi, Rombo

ZAIDI ya wakazi 2,500 wa Vijiji vya Kahe na Urauni, katika Ukanda wa Chini, Wilaya ya Rombo, mkaoni Kilimanjaro, wanalazimika kwenda nchi jirani ya Kenya kutafuta
huduma ya maji safi na salama ambayo hawaipati katika vijiji hivyo.

Akizungumza na Majira jana, Mhandisi wa maji katika Halmashauri hiyo Bw. Andrew Tesha, alisema vijiji tisa vya ukanda wa chini, vinakabiliwa na tatizo la uhaba wa maji kwa muda mrefu kutokana na sababu za kijiografia.

Alisema hali hiyo inachangia kukwamisha huduma mbalimbali za mkijamii kwani wananchi hulazimika kutumia muda mwingi kutafuta huduma hiyo.

“Mtu anaweza kutembea umbali wa saa nne au tano kwenda nchi jirani ya Kenya kutafuta huduma ya maji, hii ni aibu kubwa kwa Taifa letu hasa tunapoelekea katika maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru,” alisema Mhandisi Tesha.

Kwa upande wake, mbunge wa jimbo hilo Bw. Joseph Selasini, alikiri kuwepo kwa hali hiyo na kuongeza kuwa, tayari hatua za kupambana na adha hiyo zimeanza kuchukuliwa.

Alisema ukanda wa chini katika jimbo hilo, unakabiliwa na tatizo kubwa la maji ambalo limedumu muda mrefu kutokana na vyanzo vingi vya maji kuwa nje ya halmashauri.

“Kero hii inafahamika, tunatarajia kuchimba visima ili kukabiliana na tatizo hili, siku chache zijazo mambo yatakuwa mazuri,” alisema.

No comments:

Post a Comment