*Aapa kamwe hatakubali serikali kuilipa Dowans
*Asema iliirithi Richmond isiyotambuliwa kisheria
*Wanaharakati watangaza siku 10 za maandamano
*Yaelezwa TANESCO kukata rufaa changa la macho
Na Waandishi Wetu
SIKU chache baada ya Mahakama Kuu kusajili tuzo ya malipo ya sh. bilioni 94 ambazo
Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) linapaswa kuilipa kampuni ya Dowans, Waziri wa Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bw. Samuel Sitta amesema katu hawezi kukubaliana na malipo hayo kwa kampuni ambayo ni haramu nchini.
Bw. Sitta ambaye kwa muda mrefu amekuwa akipinga serikali kuilipa kampuni hiyo, alitoa kauli hiyo juzi alipokuwa akihojiwa kwenye kipindi cha Keki ya Taifa kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha Mlimani, mada ikiwa ni miaka 50 ya maendeleo na changamoto ya uadilifu.
Alisema miongoni mwa sababu zinazomfanya kuonesha msimamo huo ni kwa sababu kampuni hiyo ni haramu kwa kuwa ilirithishwa mikoba na kampuni ya Richmond, ambayo haitambuliwi na Sheria ya Manunuzi nchini pamoja wala Mamla ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).
Akizungumzia kuwamo ndani ya serikali anayoikosoa, alisema, "Baadhi ya mambo tumeyaepusha yasijirudie kiuzembe kwa sababu tupo na tunayafuatilia kwa karibu, kama tusingekuwa serikalini na kuonesha misimamo yetu bila kujali tupo ndani kuna mambo yasingepata suluhisho, ndiyo maana wengine tunasema hakuna haja hata kidogo ya kuilipa hata senti moja kampuni haramu ya Dowans
Hivyo, tuvute subira kwa kuwa serikali ipo katika hatua ya kukata rufaa ya tuzo hiyo, mambo huenda yakawa mazuri na kama hayatakuwa mazuri tutafahamu la kufanya wakati huo," alisema Bw. Sitta.
Aliongeza kuwa jambo la kushangaza kampuni hiyo ya Dowans wakati ikiendelea kufuatilia tuzo hiyo, imeiuza mitambo yake kwa kampuni ya Symbion kwa gharama kubwa zaidi, na suala hilo haliwezi kufumbiwa macho akiwa miongoni mwa wanaharakati wanaopinga ulipaji wa fedha hizo.
"Dowans wameuza mitambo yao kwa kampuni ya kuzalisha umeme ya Symbion mara dufu zaidi, kiasi cha dola milioni 120, hivyo hatuwezi kuwafumbia macho watu waovu kwa kuwa ndani ya sheria zetu hamna sehemu inayoruhusu kuwepo kampuni haramu kama hii," alisema Bw. Sitta.
Alisema Richmond ni utaratibu wa kijanja na ndio maana hawakufuata taratibu zozote, na kwamba vigezo ambavyo waliviweka TANESCO vya mzabuni vilikuwa 24 lakini vilipunguzwa hadi kubakia vinne ili kuipitisha.
“Dowans ni biashara ya kipumbavu…nawashangaa hata hao wanaotulaumu sisi kuwa ndio tumeifikisha nchi katika hatua hiyo ya kutakiwa kulipa deni hilo, Dowans ni wizi na kila Mtanzania anapaswa kulaani ushenzi huo badala ya kushangilia,” alisema.
Alisema kuwa Tanzania iliingia mkataba na Kampuni ya Richmond ili ifue na kuzalisha umeme lakini cha ajabu humo humo kukafanyika wizi na mkataba huo hewa wakarithishwa Dowans.
"Dowans hatukuwapa mkataba bali walirithi uharamu wa kampuni hewa, hivyo hatuwezi kubebesha wananchi matatizo ya uharamu halafu tukashangilia kuibiwa,” alisema.
"Dowans ni wajanja, wamecheza mchezo katika makaratasi, kitu ambacho ukikaa chini na kukichunguza kwa makini utagundua kuwa tumelipa mamilioni ya fedha bila ya sababu za msingi," alisema.
Mabadiliko ndani ya CCM
Bw. Sitta alisema iwapo itafikia mahali na kugundua kwamba yale ambayo yanapangwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) hususani kufanya mabadiliko ya haraka ili kuokoa jahazi, kwa upande wake atafanya maamuzi ambayo anaona ni sahihi kwa manufaa ya Watanzania.
"Tangu Oktoba 5, 1960 mimi nilikuwa mwanachama rasmi wa Chama cha TANU hadi kuwa CCM mwaka 1977, ninatambua mengi ambayo tulikuwa tunafanya enzi za TANU kwa sasa hayatekelezeki kwa manufaa ya Watanzania na ilifika mahali nikaanza kuandamwa sana, kutokana na misimamo yangu, ndiyo maana ikifika mahali nikiona hamna mabadiliko CCM, kwa upande wangu ninaweza kuchukua maamuzi.
"Ukizingatia kipindi hicho chote utagundua ndani ya chama nina zaidi ya miaka 50, hivyo wale wanaoona nijiuzulu madaraka, ikifikia hatua ya kufanya hivyo nitajuzulu lakini bado, ninatambua ndani ya CCM kuna watu wenye uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko iwapo tutafunga mikanda na kudhamiria kuwatetea Watanzania kisawa sawa," aliongeza.
Uchaguzi Igunga
Akitoa tathimini yake juu ya uchaguzi mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Igunga, alisema ushindi ambao CCM iliupata siyo jambo la kujivunia, bali inapaswa kujipanga sawa sawa kwa kuwa matokeo hayo yaliashiria taa ya njano.
"Kura zetu jimbo la Igunga si jambo la kujivunia hasa ukizingatia kwamba zaidi ya asilimia 55 ya kura ndiyo ushindi wetu huku CHADEMA kikichukua nafasi ya pili kwa zaidi ya asilimia 40, hiyo ni ishara ya taa ya njano ambayo inapaswa kufanyiwa kazi haraka na viongozi wa chama chetu kabla mambo hayajawa mengine," alisema.
Wanaharakati kuandamana
Msimamo wa Bw. Sitta unaungwa mkono na wanaharakati ambao wameamua kupinga malipo hayo barabarani, kwa watu kuandamana kwa amani
nchi nzima, na wamewataka Watanzania kutumia ibada za Ijumaa, Jumamosi na Jumapili wiki hii kuomba ujasiri wa kutetea nchi yao.
Katika maandamano hayo, waandamanaji wametakiwa kutumia muda wa siku kumi kuvaa vitambaa vyeusi mikononi na bendera za taifa shingoni au kichwani, ikiwa ni ishara ya kutokukubaliana na ufisadi
unaofanyika nchini na kuishinikiza serikali kutolipa fedha hizo.
Wanaharakati hao wanadai kuwa hiyo ndiyo njia pekee ambayo Watanzania wanaopinga harufu ya ufisadi inayodaiwa kuzunguka sakata hilo, wamebakiwa nayo, kwani kwa mujibu wa mkataba wa kampuni tata ya Richmond na TANESCO, uliorithiwa na Dowans, hukumu
iliyotolewa na Mahakama Kuu mapema mwezi huu na kusajili tuzo hiyo, ilikuwa ndiyo fursa ya mwisho kwa utaratibu wa kimahakama.
Kifungu cha 14 cha hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC) kinaeleza bayana namna pande hizo mbili zilivyokubaliana kuwa maamuzi ya msuluhishi huyo yatakuwa ni ya mwisho na yanapaswa kuheshimiwa na pande zote mbili, hivyo hakuna upande utaweza kukata rufaa mara baada ya mahakama kuu kutoa uamuzi wa kusajili tuzo hiyo.
Maandamano hayo yameitishwa nchi nzima Oktoba 14, ambayo huwa ni siku ya maombolezo ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye baada ya kufariki dunia alizikwa baada ya siku 10. Hivyo muda huo ndiyo utakaotumika kupinga Dowans na ufisadi mwingine wa mali za umma nchini.
Wanaharakati hao ni Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), HakiElimu, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Agenda Participation 2000, SIKIKA Tanzania na HDT.
"Jambo hili limetusikitisha sana kwa kuwa serikali kama mlinzi wa rasilimali za umma ametusaliti au ameshirikiana na wezi kuiba au kutumia vibaya rasilimali za umma. Pia hali hii inaonesha dhahiri kuwa kuna viongozi wa serikali wanaonufaika na watakaogawana rasilimali hii. Tokea mwanzo umma haukushiriki katika kujua kuwa TANESCO imeshtakiwa kwa kuingia katika mikataba mibaya.
"Pia linadhihirisha kuwa serikali imedhamiria kulipa tuzo ya Dowans. Hii inatupa maswali maswali mengi; Je, Dowans ni nani mpaka serikali inamlinda hivyo? Je, malipo hayo analipwa nani? Na yanatoka katika kipengele kipi cha bajeti ya serikali? Ni hatua gani imechukuliwa dhidi ya waliotuingiza katika mkataba huu?" alihoji Bw. Irenei Kiria, Mkurugenzi Mtendaji wa SIKIKA alipokuwa akitoa tamko hilo kwa niaba ya wenzake.
"Tunatoa wito kwa Watanzania wote tuadhimishe kifo cha Baba wa Taifa, kwa kuvaa nguo nyeusi, siku ya maombolezo kuanzia Oktoba 14 hadi 23 alipozikwa, tukikumbuka msimamo wake wa kupinga ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali za taifa...wananchi wote
ambao ndiyo walipa kodi ambao hawajapendezwa na mlolongo huu na ufisadi mwingine wajiandae, wawe na uthubutu na kujitokeza kwa wingi kusimamia haki zao," aliongeza Bw. Kiria.
"Uamuzi wa TANESCO kwenda mahakamani kukata rufaa ni danganya toto tu...tunapigwa changa la macho hapa walishakubaliana kuwa hawatashtakiana katika mahakama yoyote Tanzania na imeelezwa pia katika hukumu ya ICC kuwa hakuna upande utakata rufaa juu ya maamuzi hayo baada ya mahakama kuu kukubali tuzo. Kwa hiyo hapo tumefika mwisho hatutarajii uamuzi tofauti.
"Maamuzi sasa ni kwa wananchi. Katiba iko chini ya wananchi maana katika nchi za kidemokrasia wananchi ndiyo wanatunga katiba. Katiba inatasfiriwa katika sheria, sheria katika kanuni na kanuni katika miongozo mbalimbali. Kifungu cha 27 cha katiba yetu pamoja na ubovu wake, kinatoa mamlaka kwa wananchi kulinda rasilimali za nchi. Hivyo tunawaomba Watanzania kutumia wiki hiyo kupinga suala hili na ufisadi mwingine nchini," alisema Bw. Marcos Albany kutoka LHRC.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TAMWA, Bi. Ananilea Nkya alisema kuwa alisema kuwa yako makundi mbalimbali ya kijamii nchini yanaidai serikali, akitolea mifano ya walimu na wastaafu wa Afrika Mashariki, lakini serikali haijawahi kuonekana kuharakisha kuwalipa kama inavyofanyika kwa Dowans. Akaongeza kuwa Watanzania wanalodai kubwa la kuboreshewa maisha yao, lakini hawajawahi kutimiziwa na serikali.
Tanesco yakata rufaa
Wakati malipo ya Dowans yakipingwa kila kona, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupitia kwa mawakili mawake leo inatarajiwa kuwasilisha ombi la kukata rufaa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaa kupinga uamuzi wa kuilipa sh. bilioni 94 kampuni ya kufufua umeme ya Dowans Tanzania.
Akizungumza kwa waandishi wa habari kwa njia ya simu, mmoja wa mawakili hao, Dkt. Hawa Sinare alisema kwa sasa wapo katika hatua za mwisho kukamilisha hati ya ombi hilo.
Septemba 28, mwaka huu Mahakama Kuu ilitoa uamuzi wa kusajiliwa kwa tuzo ya kampuni ya Dowas inayoitaka TANESCO kulipa mabilioni hayo ya fedha.
Uwamuzi huo ulitolewa mahakamani hapo na Jaji Emilian Mushi wa mahakama hiyo baada ya kusikiliza na kujilizisha na hoja za pande zote mbili na kuweka wazi kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kutengua makubaliano ya mkataba waliojiwekea kati ya Dowans na Tanesco.
Miongoni mwa makubaliano hayo ni kuwa masuala yote ya kisheria yatasuluhishwa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC) na uamuzi utakaotolewa na mahakama hiyo utakuwa wa mwisho.
Habari hii imeandikwa na Godfrey Ismaily, Gladness Mbona, Stella Aron, Tumaini Makene na Rehema Mohamed.
Dah!!! mpaka kichefuchefu mh!! nchi imeoza hii
ReplyDeletesita fanya maamuzi sasa!!! usiwalee hao watakufanya kama mdogo wako mwakyembe na kolimba!
ReplyDeleteSitta, if you are a genuine person, why keep on staying in such a rotten party. I think its time for you to move on!
ReplyDeletewhy wait for a black Jesus with a party as rotten as CCM?Is CCM a political Party or is it a den of thieves who want to replenish all of the remaining resources Tanzania Habours???Where are the Leaders who had nobility to stand against evil for the betterment of their people??Awake Tanzania,it has been 50 years now and its about time this country starts a new era,it is time for Change.
ReplyDeleteccm inaitakia nchi yetu mabaya.Hivi hawajui nchi imeshazinduka?kwa nini hawajifunzi kwa yalotokea libya? au wanaona watanzania bado wamo gizani hadi sasa kwa hiyo wanadanganyika kwa oungo wowote unaotungwa na mafisadi? ipo siku watu watachoka na yatakayotokea anaju a Mungu tu.
ReplyDelete