13 October 2011

David Haye afikiria kustaafu

LONDON, England

BINGWA wa zamani wa uzani wa juu katika ngumi za kulipwa, David Haye amesema anatazamia kustaafu ngumi baada ya bodi inayoongoza mchezo huo nchini Uingereza kutangaza
kutoongeza muda wa leseni yake.

Haye, ambaye alishatangaza kwamba hatapigana tena baada ya kutimiza umri wa miaka 31, ambayo inaangukia leo alipoteza taji lake la WBA, baada ya Julai mwaka huu kupigwa kwa pointi na bondia Vladimir Klitschko.

"Naweza kuthibitisha kwamba Haye hataongeza muda wa leseni yake," Katibu Mkuu wa Bodi ya Ngumi, Robert Smith aliwaambia waandishi wa habari kwa mujibu wa gazeti la Buenos Aires Herald la Argentina.

Tangazo la bondia huyo kustaafu ngumi, limehojiwa na kambi ya Klitschko huku promota Bernd Boente, akisema kuwa muda mfupi alikuwa amefanya mazungumzo na Meneja wa Haye, Adam Booth na kumweleza kuwa bondia huyo Mwingereza, angerejea ulingoni kama kutakuwa na pambano baina yake na akina Klitschko.

"Uamuzi upo mahali hapo. Na hii inategemea biashara zaidi," aliiambia Sky Sports News. "Bado tuna mawasiliano na tunachongoja ni idadi ya vituo vya televisheni Uingereza, kama biashara itakuwa na maslahi.

Alisema kaka yake Vladimir, Vitali, ambaye ni bingwa wa uzani wa juu wa WBC anapenda mpinzani kama huyo na endapo pambano litafanikiwa, litakuwa ni kati ya Februari ama Machi mwakani.

No comments:

Post a Comment