Na Mwali Ibrahim
SHIRIKISHO la Kimataifa la Judo (IJF), limesogeza mbele tarehe ya kuanza kozi ya makocha wa daraja la pili ya mchezo huo hapa
nchini ambayo sasa itaanza Novemba 4 hadi 14, mwaka huu katika Shule ya Sekondari ya Filbert Bayi, Kibaha mkoani Pwani.
Awali kozi hiyo ilipangwa kuanza leo, lakini imeshindikana baada ya Mkufunzi wa kutoka IJF, Mfaransa Fredric Fauillet kupata udhuru, hivyo kushindwa kufika kwa ajili ya mafunzo hayo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Chama cha Judo Tanzania (JATA), Kashinde Shabani alisema baada ya mkufunzi huyo kushindwa kuwasili, IJF waliamua kusogeza mafunzo hayo mbele ambapo wamemchagua Mfaransa mwingine Hassen Iklef.
"Wao ndiyo wametutafutia mkufunzi wa mara ya kwanza, lakini baada ya kuona anaudhuru walitushauri kuisogeza mbele kozi hiyo na kupendekeza tarehe hizo, ambazo wao waliona zinafaa," alisema.
Alisema katika kozi hiyo, wapo makocha ambao tayari wameshapata mafunzo ya daraja la kwanza, yaliyofanyika mwaka 2003 na wapo ambao hawajapata, hivyo watahakikisha wote wanapata mafunzo hayo ya daraja la pili.
Aliongeza kuwa ili kuhakikisha makocha ambao hawajapa mafunzo hayo ya daraja la kwanza, wanakwenda sawa na wenzao kwani JATA itatoa mafunzo ya awali kwa wale waliokosa kufanya mwaka 2003, ambayo yatafanyika Oktoba 26 hadi 30 mwaka huu katika Ukumbi wa Ukonga Magereza, Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment