13 October 2011

Savio yazinduka, yaichapa Vijana

Na Amina Athumani

TIMU ya mpira wa kikapu ya Savio, imezinduka usiingizini baada ya kuichapa Vijana kwa pointi 63-53 katika mwendelezo wa mashindano ya mpira wa kikapu ya
Kanda ya Tano.

Savio ambayo juzi ilitandikwa na timu ya KCB ya Kenya kwa pointi 49-34, iliiadhibu Vijana katika mchezo ambao ulizikutanisha timu zote za Tanzania.

Wakati Savio, ikishangilia ushindi huo ndugu zao ABC walipokea kipigo kikali kutoka kwa timu ya Co-operative Bank ya Kenya cha pointi 77-33.

Kutokana na vipigo hivyo, hadi sasa kati ya timu nne za Tanzania zinazoiwakilisha nchi kwenye michuano hiyo ni timu moja tu ya wanawake ya Jeshi Stars, ndiyo ambayo haijapoteza mchezo hata mmoja hadi sasa.

Savio na ABC, tayari zimepoteza mechi moja na kushinda moja kila moja, huku Vijana ikiwa tayari imepoteza mechi zote mbili ilizocheza.

Katika michezo mingine ilizikutanisha timu za wageni ambapo Ethiopia, iliichakaza Rwanda kwa pointi 62-48 katika mchezo wa wanaume na kwa wanawake Ethiopia ilifungwa na Burundi kwa pointi 58-36.

Mchezo wa nne, ambao ulizikutanisha timu zote za Kenya, KTC iliichakaza KTA kwa pointi 55-53 huku APR ya Rwanda ikiionesha kazi KCB kwa kuicharaza pointi 71-67.

Mechi hizo zinatarajia kuendelea tena leo katika viwanja viwili tofauti, ambazo zote zitaanza saa sita mchana katika viwanja vya Donbosco na Uwanja wa ndani wa Taifa, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment