18 October 2011

Msikosoe kila kitu kinachofanywa na serikali-Waziri

Nickson Mahundi na Mariam Bokero

SERIKALI imewataka wadau wa maendeleo hususan mashirika yasikuwa ya kiserikali (NGOs) kuacha tabia ya kulaumu na
kukosoa kila jambo badala yake watoe mawazo ya kuboresa na kusaidiana na serikali katika kusukuma maendeleo ya taifa.

Ushauri ulitolewa Dar es Salaam jana na Waziri wa Muungano Ofisi ya Makamu wa Rais Bi.Samia Hassan Suruhu, wakati akifungua mdahalo wa Katiba Mpya ulioandaliwa na NGOS mbalimbali kwa lengo la kuwawezesha wananhi kutoa mawazo yao kuhusu maandalizi ya Katiba.

Pia aliwataka wadau hao wa maendeleo kuacha jazba wanapochangia mada katika mdahalo huo badala yake wajenge hoja ili zifanyiwe kazi kwa serikali na kuonya kuwa mtu akitumia jazba anaweza kueleweka vibaya hata kama ana mawazo mazuri.

Aliyataka mashirika hayo kufanya kazi kuanzia ngazi ya vijiji kwa uadilifu badala ya kuelekeza lawama kwa serikali ili kuleta maendeleo na kuyaenzi maelendeleo yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 50 ya uhuru wa Tanzania bara.

Kwa upande wao Asasi hizo ziliweka wazi umuhimu wa Katiba Mpya kutoa fursa kwa makundi maalumu kumiliki Ardhi na kutoa usawa na mgawanyo wa rasilimali za nchi kwa maufaa ya taifa na si kwa wawekeazaji pekee.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake Mwenyekiti wa Asasi inayojihusisha na Kuratibu Masuala ya Kupambana na Umaskini nchini  (GCAP), Bi.Martha Kabisama, alitaja ujumbe wa mdahalo huo kuwa ni 'Tanzania tunayohitaji Miaka 50 ijayo'.

Alisema Katiba mpya inatakiwa kuweka vipaumbele vya haki za mwanamke na makundi maalumu ili kutoa fursa kwao kumiliki ardhi kwa maelezo kuwa hadi sasa ni asilimia 19 ya wanawake ndio wanaomiliki ardhi ukilinganisha na wanaume.

No comments:

Post a Comment