10 October 2011

Mafuta ya taa, dizeli yapaa, Petroli yashuka

Na Mwandishi Wetu

BEI za jumla na rejareja kwa aina zote za mafuta nchini, zimebadilika huku bei ya petroli ikishuka lakini ile ya mafuta ya taa na diseli ikipanda ikilinganishwa na bei elekezi ya toleo
 lililopita.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ilieleza kuwa bei hizo mpya zinaanza kutumika leo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo petroli imeshuka kwa sh. 38.35 kwa lita sawa na asilimia 1.82, dizeli imepanda kwa sh. 16.95 kwa lita sawa na asilimia 0.85 na mafuta ya taa imepanda kwa sh. 9.35 kwa lita, sawa na asilimia 0.48.

"Mabadiliko haya ya bei za mafuta hapa nchini yametokana na kushuka kwa bei katika soko la dunia na kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania ikilinganishwa na dola ya Marekani," ilieleza taarifa hiyo iliyosainiwa Ofisa Uhusiano, Bw. Titus Kaguo.

Alisema bei za aina zote za mafuta zingeshuka kama thamani ya shilingi isingeendelea kushuka ikilinganishwa na dola ya Marekani.
Alieleza kwenye taarifa hiyo kuwa kwa kulinganisha toleo hili na toleo lililopita thamani ya shilingi katika toleo hili imepungua kwa asilimia 1.96. 
"Bei za jumla kwa kulinganisha matoleo haya mawili zimebadilika," ilisema taarifa hiyo ya Bw. Kaguo.
Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2008, bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko.

"EWURA itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei za kikomo cha bidhaa za mafuta... taarifa hizi zina lengo la kuwasaidia wadau kufanya maamuzi stahiki kuhusu manunuzi ya bidhaa za mafuta," alieleza taarifa hiyo.

Alisema  kampuni za mafuta zipo huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani ili mradi bei hizo ziko chini ya bei kikomo.
"Vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana na yakionyesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika," ilieleza taarifa hiyo.

Wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta kutoka kwenye vituo vinavyouza mafuta kwa bei ndogo zaidi ili kushamirisha ushindani.

No comments:

Post a Comment