*Nape alia wana mkakati kutenganisha urais, uenyekiti
*Asema wanatumia pesa nyingi kufanikisha malengo yao
*Adai walipanga washindwe uchaguzi Igunga, wakakwama
Na Agnes Mwaijega
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema ndani yake kuna kikundi cha waasi chenye nguvu ya
pesa ambacho kinasaidia kuupa nguvu upinzani na kuandaa mkakati wa kutenganisha cheo cha urais na uenyekiti wa taifa wa chama.
Kulingana na utaratibu CCM iliojiwekea, Rais anayekuwa madarakani ndiye anakuwa mwenyekiti wa chama hicho, hatua inayompa nguvu za kuongoza chama hicho kama sehemu ya dola.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Bw. Nape Nnauye alisema Dar es Salaam jana kuwa chama hicho kinafahamu na kufuatilia kwa makini kila jitihada zinazofanywa na waasi hao za kutaka kumhujumu Mwenyekiti wao, Rais Jakaya Kikwete.
Kwa mujibu wa Nnauye, miongoni mwa juhudi zinazofanywa na waasi hao ambao hakuwataja kwa majina, lakini habari za ndani zikiwaja wale wanaotakiwa kujivua uongozi kutokana na tuhuma za ufisadi, ni kupotosha maamuzi ya chama na kushawishi wajumbe wa vikao kuyabadili hasa ile dhana ya kujivua gamba.
Habari zilizopatikana ndani ya chama hicho, zilisema kuwa harakati za waasi hao wenye nia ya kuchukua madaraka ya nchi mwaka 2015, zimepamba moto hivi sasa baada ya kuhisi kuwa shughuli ya kuvuana magamba inaweza kufanyika wakati wowote sasa kitakaketi kikao cha NEC, baada ya kusimama kwa muda kupisha uchaguzi mdogo wa Igunga.
Hata hivyo, Nnauye alisema mipango mingi ya waasi hao inashindikana kwa kuwa uongozi wa chama unaijua mapema.
"Kwa upande wao mambo yamekwenda kinyume na dua zao, kwa hiyo na mimi nawapa changamoto kwa kuwataka watoke wenyewe hadharani kutoa madai yao badala ya kuwatumia watu, alisema Nnauye.
Alihoji kama hoja ya kutenganisha hizo kofia, urais na uenyekiti, ina maslahi kwa chama na si kwa kikundi kidogo, kwa nini wanatumia nguvu ya pesa kutaka kushawishi wajumbe badala ya kuileta kwenye vikao ili ijadiliwe?
Bw. Nnauye alisema mwenendo wa kisiasa nchini kwa sasa unadhihirisha wazi kwamba upinzani hauna nguvu kiasi hicho, ila unapewa nguvu waliyonayo wanakikundi hao wanaojiita wana-CCM lakini kwa ukweli ni waasi, na wengi wao walianza kuasi imani ya chama hicho na sasa wanaendesha kampeni ya watu kuasi maamuzi halali ya vikao vya chama chetu," alisema.
Bw. Nanuye alisema juhudi za kujaribu kuhujumu mageuzi hayo ndani ya chama hicho zimekuwepo kwa muda mrefu na wamejitahidi kuzipuuza lakini sasa umefika wakati kwa wana-CCM na Watanzania kujua ukweli.
"Wanaofanya juhudi hizi wao kiukweli wanadhani hatuzifahamu kwa sababu wanaona tumekaa kimya wakati wakicheza hizo sarakasi za kujaribu kuupotosha umma wa Watanzania," alisema.
Kushindwa Igunga
Bw. Nnauye alisema chama kinafahamu fika juhudi hizo na hivi karibuni katika uchaguzi wa jimbo la Igunga zilifanyika bila kificho, na zilisukumwa na uroho, ubinafsi na zikiwa na ujasiri mkubwa wa kifisadi bila kujali maslahi mapana ya chama hicho na nchi kwa ujumla.
"Juhudi za hivi karibuni ni kutaka chama kishingwe Igunga ili kujaribu kuhalalisha hoja ya kwamba mageuzi tuyafanyayo hayana tija kwa chama.
"Walikwenda na kaulimbiu 'Igunga tushindwe ili tuheshimiane', wakasahamu chama ni taasisi si mtu, ushindi ule wa igunga na kwenye kata mbalimbali ni ushindi wa CCM na wapenda nchi hii wote. Hivyo badi 'tumeshinda ili tuheshimiane'," alitamba Bw. Nnauye.
Pia alisema baada ya juhudi hizo kushindwa sasa wanaanza kujaribu kutumia watu mbalimbali kuimba wimbo wao wa zamani, kwamba tunapotosha dhana ya kujivua gamba bila kusema usahihi upi kama tunachokifanya ni kupotosha.
Kwa mujibu wa Bw. Nnauye, vikao vya Kamati Kuu vimeshakaa karibu mara mbili na vyote vimepongeza utekelezaji wa mageuzi hayo ndani ya CCM.
"Mapema mwaka huu Baraza Kuu la UVCCM taifa chini ya uenyekiti wa Makamu wake lilitoa taarifa kwa vyombo vya habari kupongeza utekelezaji wa maazimio ya NEC. Tujiulize,...hawa wanaodai tunapotosha maamuzi ya NEC ni akina nani na kwa maslahi ya nani?" alihoji.
Alitoa wito kwa wana-CCM kutulia na kupuuza juhudi zinazofanywa na waasi hao, akitamba kuwa kila kinachofanywa na CCM ni kwa maslahi ya chama na nchi.
Suala la Dowans
Bw. Nnuye alipoulizwa msimamo wake kuhusu TANESCO kuilipa Kampuni ya Dowans shilingi bilioni 94 kama fidia ya kuvunja mkataba baina yao, alisema watalipinga na kuhakikisha linaundiwa kamati ya uchunguzi kama ilivyokuwa sakata la Richimond ambalo liliwavua madaraka viongozi mbalimbali wa serikali.
"Sisi tutalipinga kwa kutumia sheria na siyo maandamano kama wengine wanavyotaka kufanya kwa sababu suala lenyewe liko kisheria," alisema.
endeleeni kupiga sarakasi tu sisi tunawasubiri hoyo 2015, tena msiombee tuwe tumepigika
ReplyDeleteHakika ni kujipumbaza na kauli za kila kukicha,ndugu yangu Nape tutake tusitake chama chetu kinayumba na kinalegalega kwani
ReplyDeletetunajinadi kutafuta mchawi wakati wachawi tunao na tunawalinda si rahisi hali ya chama ni mbaya, uhasama ni mwingi na kulipizana visasi kila kukicha.Ukweli tulipotangaza kujivua gamba hatukuwa na mikakati njia ipi sahihi maana hata huo muda mliotangaza ilikuwa ni uamuzi madhubuti uchukuliwe bila kulindana na kuoneana haya tutabaki tunajilaumu na kusingizia makundi hayo makundi ndio magamba yenyewe na mnayajuwa mtaacha mpk lini? Tusubirie 2014 ndio tutimuane muone hilo vumbi lake na maporomoko ya wazi yatakapojitokeza na ikifika hapo hakuna wa kuinusuru maana wote ni walafi wa madaraka na hakuna anaejali ya wote ni ubinafsi miongoni mwetu,Tujipange mwaka 2015 kuwa wapinzani sio tena chama tawala.Na kuhusu Dowans tusijidanganye ndio hayo hayo ya kujiingiza ktk mkumbo uonekane nawe umesema ukweli mkataba baina ya Richmond na Serikali kuna kipengele kuwa masuala yote ya kimkataba yasipelekwe nje ya ICC, na hata huyo mwanasheria wa serikali hana bidii yoyote kwani anajuwa haliwezekani. Njia ni kuwabana waliosababisha hasara hii wataifishwe mali zao lilipwe hilo deni, sasa hata huyo Nape anapodai watapinga kwa kutumia sheria hivi kausoma huo mkataba au ni njia ipi atakayoipita? Ni wanafiki wa kisiasa wangenunuwa hii mitambo wakati ule kwa billion 106 ingekuwa kesi hakuna,mitambo ingekuwa ya Tanesco acheni kuleta siasa za danganya toto,msitupake mafuta ya mgongo ni sawa kujifanya wang'aa kumbe mkorogo!!
Unafiki na ukosefu wa ukweli wa JK ndio utakao mponza. THis is just the begining
ReplyDeleteMkereketwa ndani nje
ReplyDeleteKwa kweli ndugu yangu Nape hapo umepotea kidogo ni ukweli chama chetu kipendwa kimepoteza mwelekeo. HIvi hamjiulizi na kusikiliza kauli na hotuba za Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere hususani alipozungumza kuhusu Uongozi, OIC, na pale alipozungumza kuhusu wahujumu uchumi? . Jiulizeni kwanza watu hao mwalimu aliwaona kabla ya kung`atuka madarakani sasa wamejitokeza na wapo ndani ya chama na nyie mnawafahamu kwa nini msiwatimue ndani ya chama kigugumizi ni nini ndugu yangu Nape?. Tekelezeni kwa vitendo acheni kupiga kelele zisizo na tija kwa taifa.
mimi siamini hata kidogo kauli za nape ni kigeugeu....how on earth aanze kujigamba ushindi wa ccm igunga ilhali hasimu wake rostam aziz alitoa masharti walivyomwangukia kutaka akisaidie chama kishinde igunga...nape hakushiriki hata kidogo kwenye uchaguzi wa igunga hana mamlaka ya kujingamba na ushindi..ni yule yule waliomwita fisadi ndiye aliyewasaidia
ReplyDeletekatika hizo sarakasi nape naye yumo mana wananchi mnatukoroga kweli nyie ndo mmeshikilia dola hizo hela mtalipa au hamlipi ...............tukutane 2015
ReplyDeleteJamani tutoke vipi hapa?
ReplyDeleteSitaki tutoke kwa style ya libya mmmh! kwani mama yangu hatoweza kukimbia atoke manzese ila lazima tutoke hapa, maswali:
1. Tutoke vipi?
2. nani wa kututoa? (kwani yote ni mijis'i)
3. Tukitoka hapa tutaenda vipi na wapi?
Ila ni lazima tutoke na tuwatoe wote kwenye allegory of the cave.
Wewe ndugu yangu Nape, acha siasa za maji taka. Kwanza tuambie kwanini ulipigwa "stop" usikanyage Igunga kwenye kampeni. Pili tuambie kama umeusoma ule mkataba unaotufilisi sasa ndipo ujitape kwa kuupigania kisheria kama unavyodai. Ni afadhali ukijinyamazia utaheshimika zaidi kuliko kujidhalilisha hadharani kila uchao.
ReplyDeleteKUJIVUA GAMBA INABAKIA SUMU
ReplyDeleteNi jambo la kupotosha wantanzania kwa kuwadanganya kuwa kujivua gamba kutaleta faraja kwa wantanzania,hili siyo kweli kabisa,kwa sababu hiyo ni lugha ya kupumbaza watu na kuwafanya waonekane kama hawafahamu lolote,ufisadi umeletwa na CCM,na mafisadi wote wako CCM,je?hilo gamba unajivuaje?