Na Grace Ndossa
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Meck Sadik ametoa wiki mbili kwa waathirika wa milipuko ya mabomu katika eneo la Gongolamboto kwenda kuchukua hundi zao
la sivyo zilizobaki zitarudishwa hazina.
Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam jana wakati akipokea msaada kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt Parseko ole Kone kwa ajili ya waathirika wa mabomu hayo yaliyolipuka katika kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Alisema kuwa kutokana na kasi ndogo ya uchukuaji hundi za pango inashauriwa kuwa ifikapo Oktoba 30, mwaka huu hundi zote ambazo hazijachukuliwa zitarudishwa hazina.
Alisejma kuwa hadi Oktoba 15 hundi zilizolipwa ni 1,144 kwa kufuata mchanganuo wa aina tatu ambapo hundi za vyombo ni 176 ambazo zimegharimu jumla ya sh. 180,350,800; hundi kwa ajili ya ukarabati ni 938 zenye thamani ya sh. 411,797,938/50, hundi za pango ni 30 zenye thamani ya sh. 18,000,000.
Pia alisema kuwa ofisi yake inaendelea kupokea misaada mbalimbali ambayo inayotolewa na wasamaria wema, na kuwa tangu mlipuko wa mabomu ya gongo la mboto uliotokea Febuari 16 mpaka sasa wamepokea misaada ya jumla ya sh. 1,270,656,042.
"Mkoa unaendelea kutekeleza shughuli mbalimbali ili kuhakikisha shughuli hiyo inafanyika kwa ufanisi, kazi ambazo zinaendelea kwa sasa ni ulipwaji wa fidia za vyombo pango na ukarabati," alisema.
Pia alisema kuwa bado wanaendelea kushughulikia malalamiko yaliyotolewa na waathirika wa mabomu ya mbagala, na mpaka sasa wamepokea mapya 2,575.
No comments:
Post a Comment