Na Mwandishi Wetu, Moshi
WAKATI polisi wamekamata watu wanne wanaodaiwa kuvamia nyumbani kwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Cyril Chami na kumtishia maisha mama yake, mmoja wa
watuhumiwa anayedaiwa kuwa kinara wao, wametuma ujumbe kwa familia hiyo kuomba radhi na kueleza utayari wake kulipa mali zilizoibwa na kugharamia matengenezo ya uharibifu uliofanyika.
Hayo yalisemwa jana na mmoja wa jamaa wa waziri huyo ambaye hata hivyo hakutaka jina lake litajwe kutokana na kuhofia usalama wa maisha yake kwa kuwa mtuhumiwa huyo bado hajakamatwa na polisi.
Kamanda polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishina Mdaidizi Mwandamizi wa Polisi Absalom Mwakyoma amethibitisha kukamatwa kwa watu wanne kuhusiana na sakata hilo na kumtaja kinara wa kikundi hicho ambaye hajakamatwa, akifahamaika kwa jina maarufu la Askofu.
Akizungumzia sakata hilo katika Kijiji cha Manushi Sinde mtoa habari huyo alisema mtuhumiwa huyo alianza kuwasiliana naye Jumapili asubuhi akiomba kukutanishwa na mama wa Waziri Chami kwa lengo la kumuomba msamaha.
“Ni kweli tumeletewa taarifa na kiongozi mmoja wa Kijiji cha Manushi Sinde, kuwa mtu huyo anataka kuja kumuomba mama msamaha kutokana na kauli yake kuwa angemchinja kwa vile mama alimtaja kuwa ni miongoni mwa watu waliovamia
nyumbani,” alisema jamaa huyo.
“Alinipigia simu na kusema kuwa atalipa vitu vyote vilivyoibwa na kwamba atanitumia sh. milioni tano kwa njia ya M-Pesa ili zisaidie kukarabati milango iliyovunjwa nyumbani kwa waziri huyo kwenye matukio mawili mfululizo ya ujambazi yaliyofanywa wiki iliyopita," alisema ndugu huyo wa waziri.
Mtoa habari huyo aliendelea kusema kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa akimsihi sana kwa kusema kuwa amekuwa akiteseka tangu alipodaiwa kutoa tishio hilo na kwamba amekuwa mbali na familia yake kwa zaidi ya siku tatu.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na mwandishi wa habari hizi katika kijiji hicho juzi waliweka wazi kufurahishwa kwao na hatua ya polisi kuingilia kati sakata hilo kwa kile walichoeleza kuwa kikundi hicho ni hatari kwa wananchi wa eneo hilo na yale ya jirani kwa muda mrefu sasa.
“Mimi shemeji yangu aliwahi kupigwa na anayejiita mkuu wa kikundi hicho hadi mimba ikatoka na akamuonya asiende hospitali wala kutoa taarifa polisi na amekaa ndani damu inavuja, sasa ni wiki ya pili, nashukuru sasa atapata tiba,” alisema mkazi mmoja wa kijiji hicho ambaye pia hakutaka jina lake litajwe.
Alisema shemeji yake alikumbana na mkasa huo baada ya mtuhumiwa kudai kuwa amepata taarifa kutoka kwa watoa habari wake, kuwa dada huyo amekuwa akitoa maneno ya kukandia mwenendo wa mtuhumiwa huyo na kikundi chake mara kwa mara kijini hapo.
Alisema kuwa mbali na kuwapiga wanakijiji wanaofutailia nyendo zake, mtuhumiwa huyo amekuwa akitumia watu wake kuwapora mazao wanakijiji ambayo wamevuna, na hivi karubuni upekuzi ulipofanywa nyumbani kwake yalikutwa magunia zaidi ya 150 ya mahindi ambayo anadaiwa kuwapora wanakijiji.
Kamanda Mwakyoma aliwataja waliokamatwa wakihusishwa na tukio hilo kuwa ni Modest John au Bosco Malamia au mbili, (32); James Kayoyo (45); Stein Bazil (22) na Ramadhan Massawe (40), ambao alisema wote ni wakazi wa eneo hilo na TV moja imekutwa imetekelezwa migombani katika kijiji hicho.
Alisema bado jeshi hilo linawatafuta watu wawili wanaohusishwa na tukio hilo akiwamo Askofu anayetajwa kuwa ndiye kinara wa kikundi hicho na mwenzake mmoja.
Habari kutoka ndani ya jeshi hilo zinasema kuwa kukamatwa kwa watuhumiwa hao wanne kumefanywa na kikosi maalumu cha askari kutoka jijini Dar es Salaam wakisaidiana na wengine wa mjini Moshi kwa ushirikiano na raia wema wa Kijiji cha Manushi Sinde.
Mh kweli vizizi vinafanya kazi mwaka huu! kila mtu amejizatiti, hadi jamabazi anaomba radhi! ukistaajabu ya Mussa utaona ya Firauni
ReplyDeleteSomething is wrong within the government. Yaani mpaka aibiwe waziri ndipo wezi wakamatwe!
ReplyDelete