07 December 2010

Waua vikongwe, wawachoma moto

*Waliwatuhumu kuwa wachawi

Na Suleiman Abeid, Shinyanga
 JESHI la Polisi mkoani Shinyanga linawashikilia watu 10 wilayani Bukombe wakituhumiwa kuhusika na mauaji ya kikatili ya wakazi wawili wa kijiji cha Ibamba wilayani Bukombe akiwemo mwanamke kikongwe mwenye umri wa miaka 90 waliohisiwa kuwa ni wachawi.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Bw. Charles Nyanda alisema kukamatwa kwa watuhumiwa hao ambao hata hivyo hakuwataja majina, kunatokana na tukio la wanakijiji wenye hasira kuwashambulia kwa kipigo wanakijiji wenzao  na kusababisha vifo vyao na miili yao kuichoma moto.

Bw. Nyanda aliwataja waliouawa kuwa ni pamoja na Bi. Roza Kagoma (90) na Bw. Balandye Matulo (80) wote wakazi wa Kijiji cha Ibamba Kata Uyovu wilayani Bukombe mkoani Shinyanga.Bw. Nyanda alisema mauaji hayo yalitokea Desemba Mosi mwaka huu saa 5.00 asubuhi katika kijiji cha Ibamba baada ya wanakijiji hao kuwavamia wanakijiji wenzao na kuwaangamiza.

Alisema chanzo cha mauaji hayo ni imani potofu za ushirikina na kwamba mara baada ya uchunguzi juu ya tukio hilo kukamilika watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya mauaji.

1 comment:

  1. Hata kama kuna imani ya ushirikina katika jamii, ningetegemea nguvu ya dola ( polisi ) iwe karibu na jamii ili kwamba mara tu fujo za aina yoyote zikijitokeza, zinashugulikiwe mara moja kabla ya madhala kama haya kutendwa. Ni aibu kwa Taifa letu kama wananchi wanaruhusiwa kujichulia sheria mikononi mwao.

    ReplyDelete